YAS TANZANIA YAANDAA FUTARI MAALUMU KWA WATEJA WAKE ZANZIBAR

Yas Tanzania imefanya hafla maalumu ya futari na wateja wake wa Zanzibar katika
Hotel Verde, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 100 tangu mabadiliko rasmi
ya chapa kutoka Tigo, TigoZantel na Tigo Pesa kwenda Yas na Mixx by Yas.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiongozwa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa
Mjini Magharibi, Mhe. Idrissa Kitwana Mustafa, washirika wa kibiashara, wateja
wa Yas & Mixx by Yas, na wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhe. Idrissa
Kitwana Mustafa aliipongeza Yas Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kukuza
uchumi wa Zanzibar kupitia huduma za mawasiliano pamoja na huduma za kifedha
kwa njia ya simu. Vilevile alitumia fursa hiyo kuishauri Kampuni ya Yas
Tanzania kutuma jumbe za kuhamasisha amani kwa wateja wake kwakua mwaka huu ni
mwaka wa uchaguzi.

“Yas Tanzania imeendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika
kuwahudumia wateja wake na jamii ya Zanzibar kwa ujumla. Hata hivyo, kwa kuwa
mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, naomba kampuni hii itumie majukwaa yake
mbalimbali kuhamasisha amani, utulivu, na mshikamano miongoni mwa
wananchi,”
alisema Mhe. Kitwana.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa
Yas Tanzania, Ndugu Innocent Rwetabura, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mabadiliko ya chapa za Yas na
Mixx by Yas, ambayo yameleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya mawasiliano
nchini.

“Tunaposherehekea siku 100 za Yas na Mixx by Yas, tunajivunia kuwa
tumeweza kuwa karibu zaidi na wateja wetu na kuwafungulia fursa nyingi za
kidijitali. Katika kipindi hiki kifupi, tumepokea mapokezi chanya kutoka kwa
wateja wetu, na tumeendelea kuwekeza katika teknolojia na huduma bora ili
kuimarisha zaidi uzoefu wao,”
alisema Rwetabura.

Katika hotuba yake, Rwetabura alieleza
mafanikio makubwa yaliyopatikana katika siku 100 za Yas na Mixx by Yas, ikiwa
ni pamoja na:

     
Tuzo mbalimbali za umahiri: Yas imepokea
tuzo za kimataifa na kitaifa, ikiwemo kutoka kwa Ookla na TEHAMA Awards, pamoja
na kutambuliwa na TRA kama mlipaji mkubwa wa kodi katika Ushuru wa Forodha.

     
Ushirikiano wa kimkakati: Yas imeanzisha
ubia na taasisi mbalimbali kama Zanzibar Petroleum Limited (ZPL), DSE, na
e-Government Agency Zanzibar (EGAZ) ili kuimarisha huduma zake kwa Watanzania.

     
Uwekezaji katika miundombinu: Kampuni
imeongeza idadi ya minara yake nchini hadi kufikia zaidi ya 4,000 ili kuboresha
upatikanaji wa huduma za mawasiliano na intaneti yenye kasi.

      Kampeni
ya “Magift ya Kugift”: Kupitia promosheni hii, zaidi ya Watanzania
1,300 wamenufaika kwa kupata zawadi zikiwemo magari mawili mapya, zawadi za
fedha taslimu zenye thamani ya zaidi ya TZS milioni 840, na simu janja zaidi ya
540.

Rwetabura aliwashukuru wateja wa Zanzibar
kwa kuendelea kuunga mkono Yas na Mixx by Yas, akisisitiza kuwa kampuni
itaendelea kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya wateja wake.

“Zanzibar ni sehemu muhimu ya safari yetu ya kuwafungulia
Watanzania fursa za kidijitali. Tunajivunia wateja waaminifu ambao wameendelea
kuwa nasi katika mabadiliko haya makubwa. Ahadi yetu ni kuendelea kuboresha
huduma zetu ili ziwe za viwango vya kimataifa,”
aliongeza.

Katika hitimisho la hafla hiyo, Yas
Tanzania iliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kukuza uchumi wa visiwa hivyo kupitia huduma zake za kidijitali na
mawasiliano.


Related Posts