Na Seif Mangwangi, Arusha
UMOJA wa Wazazi Tanzania wa Jumuiya ya Chama cha Mapinduzi (CCM), umesema wanachama wa Jumuiya hiyo wanakiu ya uchaguzi na wako tayari kuingia kwenye uchaguzi wakati wowote licha ya kusikia kuna baadhi ya vyama vya siasa vinataka kugomea uchaguzi Mkuu ujao.
Aidha Jumuiya hiyo imeandaa kongamano kubwa la kimataifa litakaloainisha mafanikio ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 15, 2025 Jijini hapa Mwenyekiti wa Umoja wa wazazi wa Jumuiya ya CCM Taifa, MCC, Rajabu Maganya amesema kongamano hilo litafanyika Machi 22, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC Jijini Arusha.
Maganya amesema CCM ina kiu ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu 2025 na katika kuonyesha tayari yake wake imeshatoa kauli mbiu yake ya kazi na utu, tunasonga mbele na kutoa wito kwa watanzania kuepuka watu wanaotaka kususia uchaguzi mkuu.
Akizumzia kongamano hilo amesema mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakuu wa idara tofauti za Serikali pamoja na wataalam wengine watatoa mada mbalimbali kuhusu mafanikio ya Rais Dkt Samia.
” Mtakumbuka Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliapa kutumikia nchi hii, Machi 19, 2025, kwa hiyo itakapofika Machi 19 itakuwa ametimiza miaka minne kamili, hivyo tumeandaa kongamano hili ili kuonyesha watanzania na Dunia mambo mazuri aliyofanya Rais wetu,”Amesema.
Amesema kongamano hilo litatanguliwa na kikao cha kikanuni cha wajumbe wa Baraza la Jumuiya ya Umoja wa wazazi wa CCM Tanzania kitakachofanyika Machi 21, 2025 ambapo wajumbe kutoka kote nchini watahudhuria.
Maganya amesema pia katika kongamano hilo ambalo watanzania wote wanaalikwa kutakuwepo na shughuli za kijamii ambazo zitatangazwa hapo baadae.
Wakati huo huo, Maganya ametoa onyo kali kwa wanachama ambao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi kutaka kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM na kusema hakuna kiongozi anayeweza kufanya kitendo hicho.
” Hakuna maelekezo yoyote ambayo yametolewa kwa watu wanaopita huko kutaka uongozi, waache mara moja kuchafua majina ya viongozi, na tukiwabaini hawataweza kuwa salama ndani ya chama,” amesema.
Amesema hadi sasa CCM imepitisha jina la watu wawili pekee ambao ni Dkt Samia Suluhu Hassan kuwania urais wa Tanzania akiwa na mgombea mwenza Dkt Emmanuel Nchimbi pamoja na Dkt Hassan Mwinyi kuwania urais wa Zanzibar.