Dodoma. Kaburi ni nyumba ya mwisho inayoulaza mwili wa mwanadamu katika usingizi wa milele, huku dini na mila zote wakiungana katika imani kuwa waliolala humo nafsi zao huishi au siku moja watakutana nao peponi.
Miongoni mwa nyumba zinazoheshimiwa ni pamoja na kaburi ambalo umiliki na makazi yake ni mtu mmoja ambaye hawezi kuzungumza na jirani yake, licha ya ukweli wote wamepumzika kwa umbali usiozidi mita mbili au tatu.
Kwa muda mrefu kumekuwa na mabishano ya namna ya maziko, huku kila imani ikitaja misingi na misimamo yake katika maziko hasa ‘kichwa’ cha marehemu katika kaburi kinapaswa kuelekea wapi wakati anapozikwa.
Maeneo mengine kumekuwa na mwelekeo tofauti, lakini alama za vibao, misalaba, na alama nyingine kwa wasio na dini huonyesha mwelekeo wa kichwa cha marehemu alipolazwa kilielekea upande upi.
Je ni tofauti ya makabila, imani za dini?
Watu wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu jinsi ya kumsitiri marehemu, huku baadhi wakidai kuwa hawajui kitu chochote zaidi ya kuufukia mwili wa mtu chini ya ardhi bila kujali amewekwaje chini ya ardhi.
“Mimi napenda sana kwenda makaburini kuwasindikiza ndugu zetu, lakini leo ndiyo unanifumbua macho kwa swali lako. Kwa taarifa yako huwa nashuka hadi chini ya kaburi na kupokea mwili, naweka kwa maelekezo ya wazee,” amesema Robert Chiyanga.
Chiyanga (31) amekiri si mara moja au mbili amekuwa akiweka miili hiyo kwa kichwa kuelekea mashariki, lakini mara chache hulazimisha kichwa kuelekea upande wa magharibi.
Amesema wakiwa makaburini lazima awepo mzee wa umri mkubwa anayesimamia kuchimbwa kwa kaburi na atawasimamia vijana hadi mwili unapoteremshwa chini ya kaburi akitoa maelekezo ya namna wanavyopaswa kumuweka.
Kaburi linachimbwa urefu gani?
“Kwanza sina majibu ya moja kwa moja, maeneo mengine tunakutana na mwamba hivyo tunaamua kuishia mahali tunapoona tunaweza kumsitiri mwenzetu, lakini kwa baadhi ya maeneo yasiyo na mwamba huwa tunachimba kaburi ndefu walau futi sita hadi saba,” amesema.
Amefafanua kuwa hakuna sheria wala utaratibu wa kulazimisha kaburi lichimbwe kwa urefu gani na kwamba hajawahi kukutana na swali kutoka kwa kiongozi wa dini wala mila anayetaka au kuhoji urefu wa makaburi.
Chifu wa Wagogo ukanda wa Msanga, Richard Kolongo amesema ni utamaduni katika mila kwamba maziko yote lazima kichwa kitazame upande wa mashariki na siyo vinginevyo.
Kolongo amesema utaratibu huo ulikuwepo na utaendelea kuwepo isipokuwa viongozi wa dini wanakuja na misimamo na kuwapelekea kile anachodai “wanatuvuruga”
“Ukija hapa nyumbani utaliona kaburi na ndugu yangu alizikwa kwa kuelekea upande wa kusini, hii hali iliniumiza na inaendelea kuniumiza hadi leo, lakini kwa sababu alishakuwa mtu wa imani ya dini, ilibidi familia tuwe wapole,” amesema.
Kingine ametaja mabadiliko ya kisasa ambayo watu wanazikwa kwenye masanduku pia imepoteza mila na kuwafanya vijana wasijue utamaduni wao, kwani maiti wote wanazikwa wakiwa wamelala nyuso zikitazama juu, ambayo si mila ya Wagogo.
“Zamani tulipokuwa tukiwazika marehemu, ilikuwa wote wanalala vichwa kuelekea mashariki, lakini wanaume wanalala nyuso zao kuelekea kaskazini kwa maana ya kulalia mkono wa kulia na wanawake walielekeza usono kusini wakiwa wamelalia mkono wa kushoto,” amesema.
Chifu wa Wagogo kwa jamii ya Wanyanzaga, Lazaro Chihoma amesema mpango wa kubadili maziko umebadilishwa na aliowaita watu wa dini, huku akieleza kuwa mara nyingi huwa anashindwa kuwaelewa.
Chifu Chihoma amesema mila za Kiafrika hazielekezi kichwa cha marehemu upande mwingine wowote zaidi ya mashariki.
Chihoma anasema iko hivyo kwa sababu ya jua linakochomozea, wakiamini mwanzo mpya wa siku yenye nuru na ndivyo inavyokuwa mwanzo mpya wa maisha ya mwanadamu baada ya kumaliza siku zake duniani.
“Ukielekeza kichwa upande wa magharibi unataka kusema maisha ya marehemu yanakuwa gizani au ndiyo mwisho wake huo wakati imani inatueleza kuwa huyu mtu ataendelea kuishi nasi katika tumaini, na ndiyo maana tunakwenda kutambika,” anasema Chihoma.
Viongozi wa dini watofautiana
Askofu Dk Edward Mwaikali wa Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki mkoani Mbeya amesema sheria ya dini ya Kikristo ni lazima kichwa cha marehemu kielekezwe upande wa magharibi.
“Hatuhitaji kubishana, huo ni mwongozo wa neno la Mungu tangu wa Israel, ndivyo walivyozika na hadi leo wanazika hivyo, someni Biblia katika Kitabu cha Walawi mtaona hayo mambo,” amesema Dk Mwaikali.
Askofu ameeleza kuwa mwili wa mtu unapowekwa kaburini unalala kwa muda wakitegemea siku moja atafufuka na kuungana na ndugu zake ndiyo maana wanasema roho huwa iko hai, bali mwili ndiyo unakufa. Na kwa mtazamo huo, ni muhimu kulifuata jua linakokwenda.
Hata hivyo, madhehebu mengi kwa Mkoa wa Dodoma ukiacha Wilaya ya Mpwapwa, lakini maeneo mengi wanazika kuelekeza vichwa mashariki isipokuwa wachache Mpwapwa wanaelekeza magharibi.
Sheikh wa Msikiti wa Ikungi mkoani Singida, Alhaj Salum Ngaa amesema kichwa cha marehemu ni lazima kielekezwe upande wa mashariki, muhimu kulalia mkono wa kulia ili uso uelekee kaskazini.
Alhaj Ngaa amesema katika imani ya Kiislamu, wenye madhehebu mengi ndani yake, ni moja tu la Makadiria (Mabohora) ambao wanazika kwa kuwachoma moto watu wao, lakini wengine wote hawatofautiani kwenye maziko hayo.
Amesema katika hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W), wanaamini kuwa hata Nabii Ibrahim na mwanawe Isaka walizikwa hivyo, na ndiyo maana wanaendelea na maisha yao kwa namna hiyo.
Hata hivyo, mbobezi huyu katika masuala ya dini ya Kiislamu ameeleza sababu za kuelekeza uso upande wa Kaskazini kwamba huelekea upande huo ni kulenga eneo liliko jiwe la Kaabah ambalo linatajwa ni maarufu kwa ajili ya kuunguza dhambi.
“Ikumbukwe ukiwa Maka, inabidi uzikwe kichwa kielekee mashariki, lakini uso uelekee kusini, na ukiwa Madina utazikwa kichwa mashariki, lakini uso magharibi, zote tunalenga jiwe hilo ili kuondoa madhambi yetu,” amesema Alhaj Salum.
Mlinzi na msimamizi wa makaburi
Benard Ndalije, msimamizi wa Makaburi Jijini Dodoma amesema mara chache amekutana na mitazamo tofauti kwenye maziko ingawa asilimia kubwa wanazika kuelekeza vichwa upande wa mashariki.
Amesema asilimia kubwa ya wanaozika maeneo hayo ni wa kabila la Wagogo, ambao licha ya Ukristo, lakini bado wanaishi katika imani ya asili, ndiyo maana wanazika kuelekeza kichwa cha marehemu upande wa mashariki, ingawa wachache wanabadili mwelekeo.
Hata hivyo, amekiri kuwa hapajawahi kuwa na mgongano wa namna yoyote makaburini hapo kwa watu wanaotaka kuzika, kwani kila mmoja anapokuja na msimamo wake, husikilizwa na kuheshimiwa.