MIONGONI Mwa nyota wa kutazamwa kwenye kikosi cha Yanga Princess ni Neema Paul anayemudu kucheza winga zote mbili.
Paul alijiunga na Yanga msimu uliopita 2023/24 akitokea Fountain Gate Princess 2022/23.
Msimu wa kwanza akiwa na Yanga kwenye mechi 18, alifunga mabao manne na kumfanya amalize kinara wa ufungaji kwa Wananchi.
Msimu huu kwenye mechi 12 tayari kafunga mabao 12 wastani wa kuweka nyavuni bao moja kwa kila mchezo akiwania vita ya ufungaji na Jentrix Shikangwa wa Simba mwenye mabao 17 na Stumai Abdallah 21.
Hadi sasa yupo kwenye tatu bora za wafungaji na ndio kinara kwa upande wa Yanga akivunja rekodi ya msimu uliopita.
Akimzungumzia juu ya kiwango cha winga huyo, Kocha wa timu hiyo, Edna Lema alisema ni mchezaji mwenye uwezo wa kushambulia na hatari akiwa ndani ya boksi.
“Naamini kwa nafasi anayopata na viungo wanaomzunguka atakuwa bora sana mbeleni, Neema ni mchezaji mzuri na huu unaweza kuwa msimu bora kwake,” alisema Mourinho.