KOCHA wa Bigman FC, Zubery Katwila amesema licha ya kukabiliwa na ratiba ngumu katika michezo minane iliyosalia kumaliza msimu huu, ila amejipanga kuhakikisha kikosi hicho kinamaliza nafasi nne za juu ili kupata nafasi ya kucheza ‘Play-Off’.
Kauli ya Katwila inatokana na ratiba ngumu inayomkabili kwani katika michezo minane iliyobakia ni mitatu tu ya nyumbani, huku mitano ikiwa ni ya ugenini, akianza na wa jana dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara.
“Ratiba ni ngumu kwa sababu ukiangalia michezo mitano ugenini na ushindani jinsi ulivyokuwa unaona kabisa tuna kazi ya kufanya, ingawa ninachokiamini ukiwa na maandalizi bora huwa unashinda sehemu au uwanja wowote bila ya kujali mpinzani.”
Katika michezo hiyo mitano ya ugenini, mbali na mchezo wa jana na Polisi Tanzania, ila atacheza na Kiluvya United Machi 29, Transit Camp (Aprili 13), Mbuni FC (Mei Mosi) na kuhitimisha msimu kwa kupambana mechi ya mwisho na TMA FC Mei 10.
Mitatu ya nyumbani itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi, ni dhidi ya Geita Gold (Machi 23), African Sports (Aprili 19), kisha kuikaribisha Mtibwa Sugar Aprili 26, ukiwa ni mchezo utakaovuta hisia kubwa kutokana na ubora wa timu hizo.