KIPA wa Dodoma Jiji, Mkongomani Alain Ngeleka ameingia katika orodha ya makipa waliopigwa mabao mengi katika mchezo mmoja baada ya Ijumaa kufungwa sita wakati timu hiyo ikifumuliwa 6-0 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, lakini amezipotezea kiaina akisema hazitawatoa katika reli.
Ngeleka alifungwa mabao hayo kwenye Uwanja wa KMC Complex, akiungana na kipa wa KMC, Ismail Mpank aliyetunguliwa pia mabao sita wakati timu hiyo ikifungwa 6-1 na Yanga kwenye uwanja huo huo wa KMC, huku John Noble wa Fountain Gate alitunguliwa matano Yanga ikishinda 5-0.
Katika mchezo huo, Dodoma Jiji ilijikuta ikiambulia kipigo hicho kikubwa msimu huu kwa mabao yaliyofungwa na Elie Mpanzu na Steven Mukwala waliofunga bao moja kila mmoja wao, huku Jean Charles Ahoua na Kibu Denis wakitupia pia mawili mawili.
“Ni matokeo ya kuumiza, lakini sisi sio wa kwanza kufungwa mabao mengi kiasi hicho, imetusononesha wachezaji, pia tumeyachukulia kama changamoto ya kutujenga na kuleta ushindani zaidi, tutapambana zaidi michezo mingine ijayo..”
Ngeleka alisema baada ya mchezo huo, wamepewa mapumziko ya takribani siku nne kwa ajili ya kukaa na kufurahi na familia zao, ingawa kila mchezaji amepewa programu maalumu ya kuhakikisha anaiendeleza kabla ya Ligi Kuu haijarejea Aprili Mosi.
Kichapo hicho ni cha 10 kwa Dodoma Jiji msimu huu katika Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo 23, ikishinda saba na kutoka sare sita, ikishika nafasi ya nane na pointi 27, ambapo eneo la ushambuliaji limefunga mabao 22 na kuruhusu 33.
Kipa huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji msimu huu akitokea Kagera Sugar, anakumbukwa zaidi msimu wa 2022-23 wakati akiwa na kikosi cha Tabora United zamani Kitayosce, ambapo alijiwekea rekodi nzuri ya kufunga bao katika Ligi ya Championship.
Ngeleka alifunga bao pekee la kufutia machozi kwa upande wa Tabora United katika mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, ambao timu hiyo ilichapwa mabao 3-1, dhidi ya JKT Tanzania Desemba 3, 2022.
Nyota huyo kwa mara ya kwanza alitua nchini na kujiunga na Tabora United wakati inashiriki Ligi ya Championship msimu wa 2022-23, akitokea klabu ya Lumwana Radiant ya Zambia, ambapo amekuwa ni muhimili mkubwa kikosini.