Unguja. Wizara ya Afya ya Zanzibar kupitia Wakala wa Bohari ya Dawa, imeingia mkataba na Kampuni ya Hainan International Limited kwa ajili ya ujenzi wa ghala la kisasa la kuhifadhia dawa na vifaatiba.
Mkataba huo umejikita kutatua changamoto ya uhaba wa maeneo ya kuhifadhia dawa, ambao umekuwa kikwazo katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Ghala hili linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi dawa na vifaatiba kwa usalama na katika mazingira bora, hivyo kuongeza ufanisi katika usambazaji wa huduma za afya visiwani Unguja na Pemba.
Ujenzi wa ghala hili ni hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na kwa usahihi.
Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui leo Jumapili Machi 16, 2025 amesema ujenzi wa ghala unatarajiwa kujengwa Dunga Zuze kisiwani humo.
Amesema ujenzi huo wa ghala la kisasa unatarajiwa kukamilika kwa kipindi cha mwaka mmoja na utgharimu Sh27.6 bilioni.
“Ghala hilo la kisasa la kuhifadhia dawa litajengwa Dunga Zuze na ujenzi wake utagharimu Sh27.6 bilioni na unatarajiwa kukamilika kwa kipindi cha mwaka mmoja,” amesema Mazrui.
Amesema kutokana na kutokuwa na eneo kubwa la kuhifadhia dawa jambo hilo liliwalazimu kuingia gharama ya kukodi maghaala mengine ili kuhifadhia dawa.
“Kwa muda sasa tangu Wakala wa Bohari ya Dawa kupewa mamlaka ya kufanya kazi kibiashara tulikuwa tunakabiliwa na tatizo la uhaba wa eneo la kuhifadhia dawa jambo lililowalazimu kuingia gharama ya kukodi maghala mengine ili kuhifadhia dawa,” amesema Waziri Mazrui.
Amesema kukamilika kwa ghala hilo kutaifanya wakala huyo kuwa na ghala litakalokuwa na sehemu kubwa ya kuhifadhi dawa, kwa usahihi na usalama kwa sababu litaendana na sheria na utaratibu wa kimataifa wa kuhifadhi dawa.
Vilevile, Mazrui amesema hiyo ni fursa pekee itakayoongeza nguvu ya kufikia lengo la Serikali kuhakikisha wananchi wanapata dawa zinazohitajika na zenye viwango wanapofika katika vituo na hospitali mbalimbali zilizopo nchini.
Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Bohari ya Dawa Zanzibar, Abdulhalim Mohamed Mzale amesema bohari inatarajiwa kuwa na eneo kubwa litakalotumika kuhifadhi dawa na vifaa tiba vyote vinavyoingia nchini.
Amesema kupitia wakala huyo itaongeza fursa ya kuzifikia taasisi za Serikali na binafsi wanaohitaji nafasi ya kufanya kazi kibiashara.