Jina la Frank Komba sio geni na linafahamika sana na wadau wa mpira wa miguu kutokana na kile ambacho amekuwa akiufanyia mchezo huo.
Huyu ni mwamuzi msaidizi wa kimataifa wa Tanzania ambaye pia ni mtumishi wa Jeshi la Polisi huku pia akiwa Wakili kitaaluma.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Komba aliandika rekodi moja ya kibabe ambayo pengine inaweza isiwe rahisi kwa waamuzi wengi hapa nchini kuifikia au kuipiku iwe sasa au siku za usoni.
Rekodi hiyo ni kudumu na beji ya urefa ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa muda wa miaka 10 na kumfanya awe mwamuzi pekee wa sasa aliyeweza kufanya hivyo hapa nchini.
Komba anafichua kwa Spoti Mikiki Siri ya kile kilichombeba hadi akaweza kuandika rekodi hiyo tamu.
“kikubwa ni kuishi misingi ya michezo,mazoezi na kufanya kazi kwa usahihi kila wakati. Pia uvumilivu,maana kuna nyakati unavunjwa kabisa nguvu lakini kwa neema tu za Mungu na marafiki unasimama na kusonga mbele,” anasema Komba.
Refa huyo anasema kuwa uamuzi wa soka sio jambo na wanakutana na changamoto nyingi ambazo kwa refa asiye na uvumilivu anaweza kuachana nayo.
Komba anafichua kuwa mwajiri wake ambaye ni Jeshi la Polisi nchini anampa mazingira wezeshi kazini ambayo yanamfanya amudu ratiba ya kuchezesha mechi za mashindano mbalimbali.
Lakini pia anasema mawakili wenzake nao wamekuwa wakimwonyesha ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake.
“Kwanza lazima nilishukuru Jeshi la Polisi kwa kunipa nafasi ya kuendeleza kipaji changu. Wana pia ratiba rafiki inayoruhusu mazoezi,kusafiri na kuchezesha Michezo ndani na nje ya nchi, pia kwenye kazi za uwakili nashirikiana kwa karibu sana na wenzangu,” anasema refa huyo msaidizi.
Anasema kuwa uamuzi wa soka umekuwa na mafanikio makubwa kwake lakini zaidi ni kumfanya awe na mahusiano mazuri na kundi kubwa la watu ndani na nje ya nchi.
“Kwanza kufahamika sana na watu, hii imenipa maisha mazuri ya kuridhisha, na hata heshima mbele za watu, na mimi naonekana ni mtu mwenye mchango chanya katika jamii,” anasema Komba.
Mechi za heshima, atamani Kombe la Dunia
Frank Komba analiambia Spoti Mikiki kuwa amechezesha mechi ndani na nje ya nchi ambazo zimemkomaza kwa kiasi kikubwa.
“Mechi ni nyingi,Simba na Yanga zaidi ya mara 6, lakini najivunia zaidi kucheza Afcon 2021, klabu bingwa afrika robo fainali 2022, Mamelodi dhidi ya Petro de Luanda (yaweza kua mechi kubwa zaidi).
“Pia fainali ya Cecafa Kagame Cup nadhani 2021 kati ya Express ya Uganda na Bullets ya Malawi hapa Dar es Salaam,” anasema Komba.
Anasema kuwa pamoja na kuchezesha mechi hizo, ndoto zake ni kuchezesha fainali za Kombe la Dunia.
“Ndoto ya kucheza mashindano makubwa Afrika imetimia japo sijaridhika, ila ndoto ya kombe la Dunia naumia sana ipo mbali sana nami,” anasema Komba.
Anaitaja familia yake kuwa imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anafanya vyema.
“Familia ipo na mimi bega kwa bega,kabla sijaoa familia yaani wazazi walinitia moyo na kujivunia sana kazi yangu, baada ya kuoa mke wangu ndio faraja kubwa sana napopata changamoto za kazi, mabinti zangu wanapenda kazi yangu na kila mara wana Italia mechi njema,” anasema Komba.
Komba anatoa ushauri kwa marefa nchini kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu ili thamani za zipande.
“Waamuzi wajitume,na kuhahakikisha wanachezesha michezo kwa haki, vilabu hata mashabiki wanatumia gharama sana kuziendesha hizi timu, haifai kumuumiza shabiki aliyejigharamia kwenda kiwanjani,tena kwa makosa yanayohepukika…pia wajue mpira sio uadui,hii ni familia…wachezaji,makocha,viongozi na hata mashabiki tuishi nao kwa upendo,” anamalizia Komba.