Dar es Salaam. Katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya walimu wa masomo ya Sayansi shule za Sekondari, Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) imetangaza nafasi za kujitolea kwa walimu wa masomo ya Fizikia na Hesabu katika shule za sekondari mkoani Kagera.
Shule hizo ni pamoja na Sekondari ya Kagera River, Kyerwa na Luteni Jenerali Silas Mayunga.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa Machi 12, 2025 na bodi hiyo ilibaini changamoto ya walimu wa sayansi katika shule za sekondari na inatekeleza mpango wa kufadhili ufundishaji wa sayansi na hisabati, STEM Support Program (SSP) kwa kufadhili walimu wa kujitolea kwa ajili ya kufundisha masomo ya Fizikia, Kemia, Hesabu na Biolojia.
“ERB ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Ujenzi iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Usajili wa Wahandisi Sura ya 63. Bodi ina majukumu ya kudhibiti tasnia ya uhandisi kwa kuwasajili na kuwaendeleza kitaaluma.
“Bodi inatambua kuwa, uhandisi umejengwa juu ya msingi wa sayansi na hisabati. Pia, inatambua umuhimu wa usawa wa kijinsia katika taaluma kwa kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) ili kuongeza idadi ya wahandisi wanawake,” inaeleza.
Vilevile bodi imesema inaratibu mradi huo kwa ufadhili wa wadau wa maendeleo wakiongozwa na ubalozi wa kifalme wa Norway.
Ikitaja vigezo vya kujiunga bodi inaeleza: “Mwalimu awe na shahada ya kwanza ya ualimu katika masomo ya Fizikia na Hesabu. Awe tayari kufanya kazi Kagera. Waombaji wanatakiwa kufaulu usaili ili kujiunga na mpango huu wa kujitolea. Baada ya kuchaguliwa walimu wa kujitolea watalazimika kujiunga na TAeSA.
“Walimu hawa watakuwa na mikataba ya kujitolea kwa muda wa miezi sita, mkataba utaongezwa kulingana na utendaji kazi. Walimu Watalipwa posho ya kujikimu.”
Aidha, Bima ya Afya, nauli ya kwenda kituo cha kazi, nauli ya likizo na nauli ya kurudi kwao baada ya mkataba kumalizika.
Bodi imesema waombaji wanatakiwa kutuma maombi kwa njia ya barua pepe kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, [email protected] wakieleza masomo wanayoweza kufundisha pamoja na nakala ya vyeti vyao vya kitaaluma na uzoefu.
Hata hivyo bodi imesema imeanza kupokea maombi tangu Machi 14, 2025 hadi Machi 31, 2025.