Wasira awapa mbinu vijana uchaguzi mkuu 2025

Ileje. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema pazia la Uchaguzi Mkuu 2025, likifunguliwa vijana wanaojiona wanasifa wajitokeze kwenye kinyang’anyiro kugombea nafasi ya udiwani na ubunge bila kuwahofia watakaokuwa wanatetea.

Kimesema hakuna mwenye haki miliki ya kushikilia nafasi hizo kwa miaka mitano, isipokuwa leseni zinapatikana kupitia kinyang’anyiro cha kushawishi wananchi na mwenye nguvu ya kushawishi wanapata ridhaa.

Hayo yanajiri ikiwa miezi mitatu imebaki kabla ya chama hicho kuingia kwenye mchakato wa kura za maoni za kuwapata wagombea wa kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mkuu, ambapo CCM pamoja na vyama vingine 18 watakapojitokeze kuomba ridhaa kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa kwenye mkutano wa ndani wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Ileje leo Jumapili, Machi 16, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Tanzania Bara, Stephen Wasira alipokuwa akiunga mkono hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Songwe, Radiweli Mwapashi.

Msingi wa hoja ya Mwapashi amedai vijana wengi hasa katika mkoa huo wanaingiwa na uoga kukabiliana na madiwani na wabunge watakaotetea nafasi hizo katika uchaguzi ujao wakisema hawataki kuwa wasindikizaji.

“Niwaombe vijana wenzangu chukueni fomu za kugombea nafasi ya udiwani na ubunge, tunahitaji tutengeneze vijana wenye nguvu ya kujenga hoja, hata Bunge liwe na mchanganyiko wa wazee na vijana,” amesema na kuongeza:

“Kuhamasisha vijana wachukue fomu nisichukuliwe kama nawatenga waliopo madarakani, ila nataka tutengeneze vijana ili chama chetu kiendelee kupika viongozi kizazi hadi kizazi,” amesema Mwapashi.

Mwapashi amesema kwa kuwa chama hicho kina lenga kutatua shida za wananchi, vijana wasiogope kujitokeza kwenye kinyang’anyiro, bali wanatakiwa kujenga hoja na kushawishi umma ukubaliane na ajenda yake.

Akiifafanua hoja hiyo katika mkutano huo, Wasira amesema ili kada apate nafasi ndani ya chama hicho lazima apambane na kukubalika kwa wananchi, huku akisema hata wabunge na madiwani waliopo hawakugombea peke yao.

“Mwaka huu tumesema hakuna mtu kupita bila kupingwa, kwa hiyo hata watakao gombea lazima walijue hilo maana tumekubaliana kijana kama unataka kugombea muda ukija njoo jitokeze kama utakuwa msindikizaji shauri yako,” amesema Wasira.

Amesema kuelekea katika uchaguzi huo, nafasi ya udiwani na ubunge vitakuwa wazi isipokuwa nafasi ya urais pekee ambayo uamuzi ulishafanyika Dodoma na wagombea wanajulikana.

“Nafasi ya urais, mkutano mkuu maalumu ulikubali nafasi ya urais kugombewa na Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri aliyofanya ndani ya kipindi chake cha miaka minne,” amesema.

Nafasi ya mgombea mwenza alipitishwa Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho. Rais wa Zanzibar, Dk Husein Mwinyi, naye alipitishwa kuwania nafasi ya urais kwa upande wa Zanzibar.

Wasira amesema Tanzania ina vijana wengi na kazi ya CCM ni kujenga viongozi bora, kazi waliyoifanya tangu kupata uhuru, hivyo wajitokeze wakanolewe ili wawe tayari kuwatumikia wananchi.

Kulingana na Wasira, muda ukifika, kamati za siasa ngazi ya kata ziwatafutie watu wenye uwezo wa kuwania nafasi ya udiwani, sambamba na kamati za siasa wilaya, nafasi ya ubunge, waweze kupata viongozi wanaokubalika.

Kabla ya mkutano huo kufanyika, Wasira alianza kuzindua mradi wa jengo la kitega uchumi linalojengwa na chama hicho katika wilaya hiyo pia aliendesha kampeni ya kuchangisha fedha zitakazosaidia ujenzi.

Wasira yupo Mkoa wa Songwe kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho aliyoianza juzi akiwa ambeambatana na baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho.

Related Posts