Vyuo vyatakiwa kujipanga kupokea wanufaika wa mpango elimu bila ada

Dar es Salaam. Vyuo vikuu na vya kati vimetakiwa kuanza maandalizi ya kulipokea kundi la kwanza la wanafunzi wanufaika wa mpango wa elimu bila ada litakalojiunga na ngazi hizo za elimu kuanzia mwaka 2027.

Miongoni mwa maandalizi yaliyoelekezwa ni ujenzi wa miundombinu itakayowezesha kundi hilo kubwa kupata fursa katika taasisi za elimu ya juu.

Itakumbukwa mwaka 2016 Serikali ya awamu ya tano ilianza kutekeleza mpango wa elimu bila ada kwa elimu msingi kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne na mwaka 2022 mpango huo ukawagusa pia wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Akizungumza leo Mei 17, 2024 wakati wa hafla ya uwekaji saini mkataba wa ujenzi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Kagera, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyn Nombo amesema ni wakati wa kujiandaa kwa ajili ya kulipokea kundi hilo kubwa.

Ujenzi wa kampasi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET) unaohusisha upanuzi wa kampasi, uboreshaji wa miundombinu na maboresho ya mitaala kwa taasisi za elimu ya juu.

Katibu Mkuu huyo amesema ni muhimu kwa taasisi hizo za elimu ya juu kujiweka sawa kwa kuwa kutakuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi watakaojiunga na elimu hiyo kuanzia mwaka 2027.

“Kinachoenda kufanyika Kagera ni utekelezaji wa mradi lakini pia naomba iwe sehemu ya kujiandaa kupokea kundi hili kubwa, ndiyo maana nasisitiza vyuo vinapaswa kujiandaa vyema kwa sababu namba ya wanafunzi inaenda kuongezeka maradufu”

“Tunaamini kampasi hizi zinazojengwa zimewekwa katika mikoa ya kimkakati na zitasaidia kuwapokea wanafunzi hawa,” amesema Profesa Nombo.

Profesa Nombo ametumia fursa hiyo kumtaka mkandarasi anayejenga kampuni hiyo kufanya kazi yake kwa wakati na kuzingatia viwango.

 “Mtambue kuwa mna wajibu wa kisheria na wa kimaadili wa kuhakikisha mnakamilisha mradi huu kwa kadiri ya mkataba. Tumesema kuwa fungu lililotolewa kwa ajili ya shughuli hii ni kubwa. Ni lazima thamani halisi ya fedha ionekane pale majengo yatakapokabidhiwa. Hili lijidhihirishe pia kwenye ubora wa majengo na kukamilisha ujenzi kwa wakati.

 Kwa upande wake Makamu Mkuu wa UDSM,  Profesa William Anangisye amesema dira ya chuo na mpango mkakati vinalenga kufanya mageuzi ya kitaasisi yanayoendana na vipaumbele na mahitaji ya Taifa ya sasa na baadaye.

Amesema utekelezaji wa mradi wa HEET umejikita katika kuimarisha na kuboresha miundombinu, ikiwemo ukarabati mkubwa na ujenzi wa majengo mapya pamoja na kufunga vifaa vipya kwenye majengo haya. Ni katika muktadha huo, Chuo kinajipanua na kuwafikia Watanzania zaidi kwa kuanzisha kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera katika fani za kilimo na biashara.

 “Timu yetu ya wataalamu imefanya kazi kubwa ya kusanifu, kuiwasilisha kwa wadau na watumiaji wa majengo, kuifanyia marekebisho na kisha kupitishwa na Baraza. Tathmini ya Athari za Kimazingira kutokana na shughuli za mradi zilifanyika na mahitaji yake yalizingatiwa kwenye usanifu wa majengo,” amesema Profesa Anangisye.

Mratibu wa mradi  huo, Profesa Benardeta Killian amesema ujenzi huo utahusisha jingo la utawala, taaluma, bweni la wanafunzi wa kike litakalokuwa na uwezo wa kuchukua watu 70, bwalo la chakula na sehemu ya biashara.

Akizungumzia uwepo wa kampasi hiyo katika mkoa wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amesema utachangamsha uchumi na kutoa fursa za ajira.

 “Kutakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu, fursa za biashara zitakuwepo na imani yangu ajira zitazalishwa. Furaha yetu ni kwamba kampasi hii haiendi kuleta elimu tu bali fursa nyingine nyingi tutazipata.

“Ahadi yangu ni kusimamia kwa ukamilifu na kuweka mazingira wezeshi kwa mkandarasi aweze kufanya kazi yake kwa ubora ndani ya muda uliopangwa. Tumefurahishwa zaidi na aina ya mitaala itakayotolewa kwa kuwa itawawezesha vijana kujiajri,” amesema Fatma.

Ujenzi wa kampasi ya Kagera utahusisha majengo manne na utatekelezwa na mkandarasi kampuni ya China Jiangxi Corporation for International Economic and Technical Cooperation.

Ujenzi huu utafanyika ndani ya miezi 12 kuanzia sasa na utagharimu Sh13.4 bilioni kati ya Sh110 bilioni zilizotolewa kwa UDSM katika utekelezaji wa mradi wa HEET.

Related Posts