Upepo wa ubingwa Bara, mtego upo hapa!

UPEPO umebadilika. Upepo wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara umebadilika baada ya timu kadhaa zilizokuwa zikichuana na vigogo Simba na Yanga kujichuja zenyewe njiani.

Azam FC, Singida Black Stars na hata Tabora United zilizokuwa zikichuana na vigogo hivyo, kimahesabu ni kama zimekubali yaishe na mziki sasa umebaki kwa vigogo Simba na Yanga.

Hata hivyo, hata timu hizo zenyewe bado hazijawa na uhakika ni ipi itakayobeba msimu huu kutokana na mechi zilizosalia kuonekana kuwa mtego zaidi tofauti na ilivyotazamiwa hapo awali.

Kuwepo kwa kiporo cha Dabi ya Kariakoo, mechi iliyoshindwa kupigwa Machi 8 ni moja kati ya mitego katika dakika 720 za maajabu zilizosalia kwa timu hizo. Lau kama ungeshachezwa, hesabu zingekuwa wazi, iwapo timu mojawapo ingekuwa imeshinda mchezo huo, kwani alama tatu za dabi zingemweka mshindi katika nafasi nzuri.

Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo ikiwa na pointi 58, moja zaidi na ilizonazo Simba yenye 57 na kila moja imecheza mechi 22 na kusaliwa na nane, ikiwamo hiyo ya dabi. Mtego huo!

Katika mechi saba za kila timu, inaonekana kama Simba ina mteremko zaidi kwa aina ya timu inazokutana nazo, lakini hata mechi inazocheza asilimia kubwa itakuwa jijini Dar es Salaam kulinganisha na watani wao, watakaokuwa na safari katika mikoa mitatu tofauti.

Ligi imesimama kwa sasa kupisha kalenda ya FIFA kwa mechi za kimataifa kwa timu za taifa, kisha itarejea tena kuanzia Aprili Mosi hadi Mei 15 pazia litakapofungwa, lakini kuna mtego kwa Simba na Yanga katika ratiba za mechi zao, kulinganisha pia na rekodi zilizonazo nyumbani na ugenini.

Ratiba inaonyesha Yanga itacheza mechi saba ndani ya miezi miwili tofauti, yaani nne itazicheza Aprili na tatu itamalizia Mei na huu ni mtego kwao, kwani itapaswa kushinda ndani ya Aprili ili kuipa presha Simba itakayokuwa na majukumu ya mechi za kimataifa kabla ya kurejea katika Ligi mwezi Mei.

Kama Yanga itashinda mechi nne za Aprili itakusanya pointi 12 na kuifanya ifikie pointi 70, ikiwa ni 13 zaidi na ilizonazo Simba ambayo itakuwa na presha na kupambana kushinda mechi saba mfululizo za Mei ambapo wenyewe Yanga itacheza tatu tu kusaka pointi tisa za kufungia hesabu.

Pamoja na ushindani wa uwanjani, umbali ambao vikosi vya Simba na Yanga vitasafiri kwa ajili ya mechi hizo unaweza kuwa na athari kubwa kwa timu zote mbili. Safari hizi, zinaweza kuathiri ushiriki wa wachezaji na hali ya timu kwa ujumla kulingana na ratiba ilivyo na mfuatano wa mechi.

Lakini Aprili na Mei huwa ni kipindi cha mvua za masika na kwa viwanja vya mikoani ambavyo huwa vina changamoto kubwa katika hali ya hewa ya aina hiyo, na huu unaweza kuwa mtego kwa timu hizo kwa mechi za ugenini, lakini kazi ikiwa zaidi kwa Yanga itakayocheza mechi tatu za mikoani.

Hivyo sio ajabu Mei 25 bingwa akawa Simba au Yanga kutegemea na karata zitakavyochangwa kwa timu hizo, hususani baada ya kiporo cha dabi kupigwa ambacho kimeshikilia sehemu kubwa ya hatma ya ubingwa kwa timu hizo kwa msimu huu.

Wekundu wa Msimbazi wana mechi nne nyumbani, huku ikiwa rekodi isiyovutia kwani katika mechi 11 ilizocheza imeshinda nane kutoka sare mbili na kupoteza moja, lakini kwa rekodi za ugenini inaibeba kwani katika mechi 11 imeshinda 10 na kutoka sare moja kama ilivyo kwa watani wao wa Yanga.

Mteremko inayoupata ni kwamba katika mechi hizo za nyumbani inakutana na  Mashujaa, Pamba Jiji, Singida BS na Kagera Sugar, huku itakuwa Dar es Salaam dhidi ya JKT Tanzania na KMC na mchezo mmoja pekee dhidi ya KenGold ndio itasafari hadi jijini Mbeya.

Mechi dhidi ya JKT Tanzania, ambayo itachezwa kwenye Uwanja wa Isamuhyo huko Mbweni, pia itakuwa karibu na jiji la Dar es Salaam, ni safari ya dakika tano tu maana timu hizi ni majirani. Kambi ya Simba ipo Mbweni.

Pamoja na kwamba kiratiba mchezo dhidi ya KMC ambao utachezwa Mei 11, Simba itakuwa ugenini ni kama watakuwa nyumbani tu maana nao wamekuwa wakiutumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani. Utamu zaidi ni kwamba katika mechi za duru la kwanza wapinzani wote inaokutana nao katika kufungia hesabu za msimu ilizifumua, kitu kinachoiweka katika nafasi nzuri ya kukusanya pointi.

Simba iliifunga Mashujaa bao 1-0, ikailaza KMC 4-0, Kagera 5-2, JKT TZ (1-0), Pamba Jiji 1-0, Singida (1-0) na KenGold (2-0), ila ilipoteza kwa Yanga kwa bao 1-0.

Simba licha ya kuonekana kuwa na mteremko, lakini kuwa na mechi za kimataifa ikicheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, inawaongezea presha kubwa wakati itakaporejea Ligi Kuu na hasa kama Yanga itakuwa imeutumia vyema mwezi Aprili kukusanya pointi za kutosha katika mechi zao.

Ratiba ya mechi za Simba kuchezwa mfululizo ndani ya mwezi mmoja ni presha nyingine kwa Simba ambayo kama itavuka kwenda nusu fainali ya CAF itajiongezea mzigo mwingine na mtego katika ubingwa wa Bara kuwa mgumu zaidi kwao, kwani akili za wachezaji na benchi la ufundi zitakuwa huko.

Kuwa na mechi mfululizo mbali na zile za Kombe la Shirikisho (FA), kunaweza kufanya wachezaji kupata uchovu ambao unaweza kuwapunguzia kasi waliyonayo kwa sasa, lakini inaweza kuwa ni faida kubwa zaidi kwa timu kwani morali ya wachezaji itakuwa juu iwapo hakutakuwa na majeruhi kikosini.

Kwa upande yenyewe itakuwa na mechi tatu nyumbani dhidi ya Coastal Union, Namungo na Dodoma Jiji, huku ugenini ikiwa na mechi tatu za kusafiri kuifuata Tabora kuvaana na Tabora United iliyoilaza 3-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Mchezo mwingine mgumu ni dhidi ya Azam ambayo licha ya kwamba utapigwa Dar es Salaam, una kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0.

Baada ya kumaliza na Azam, Yanga itakuwa na safari ya pili mkoani hadi Manyara kwa ajili ya mchezo mwingine wa ligi dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaara. Safari hii kwa basi inachukua saa 11 na dakika 32 (kilometa 641.6) kwa ndege itapitia Arusha ambapo inachukua saa 1 na dakika 25, kisha wanachukua basi kutoka Arusha hadi Manyara, umbali wa kilometa 159, ambao unachukua takribani saa 3. Katika mechi ya kwanza Yanga ilishinda 5-0 ikiwa nyumbani.

Safari ya mwisho mkoani kwa Yanga itakuwa ni ya jijini Mbeya kuifuata Tanzania Prisons.

Katika mechi ya kwanza Yanga ilishinda mabao 4-0, hivyo haitakuwa na preha kubwa kwa vile hata rekodi za ugenini Yanga imefunika kwa kucheza 11 na kushinda 10, ikitoka sare moja bila kupoteza, hata hivyo kwa mechi za nyumbani dhidi ya Coastal Union, Namungo na Dodoma Jiji ambazo ilizitambia mechi za duru la kwanza sio nyepesi kwani rekodi za nyumbani zinaiangusha Yanga. Katika mechi 11 ilizocheza imeshinda tisa na kupoteza mbili, hali inayoiweka timu hiyo katika mtego.

Kwa mechi hizo za ugenini, Yanga inaweza kukutana na hali ya mvua ambazo huwa zinatibua viwanja vingi vya mikoani na kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kushindwa kucheza katika ubora uliozoeleka.

Yanga inakutana na timu hizo zikiwa zimeimarishwa katika dirisha dogo kulinganisha na ilivyokuwa katika duru la kwanza, lakini kuwa na mechi dhidi ya Azam na Tabora United ni mtego mwingine kwa kocha Hamdi Miloud, kutokana na ukweli hizo ndizo zilizoitibulia rekodi ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza wala kuruhusu bao. Azam ilianza kwa kuifunga 1-0 kisha Tabora kutonesha kidonda kwa mabao 3-1, ikiwa ni kipigo kikubwa cha kwanza kwa Yanga tangu Januari 15, 2020 ilipocharazwa 3-0 nyumbani na Kagera Sugar.

Kushindwa kukusanya pointi 12 katika mechi nne za Aprili, zitaweza kuipa Yanga presha kwa mechi za Mei wakati Simba itakaporejea kutoka jukumu la kimataifa.

Kiujumla, dakika 720 za mechi zao nane, ikiwamo ya dabi ndio zitaamua nani bingwa.

Nyota wa zamani wa Yanga, Credo Mwaipopo alisema; “Nadhani mechi za mwisho zitakuwa na mvuto sana. Safari ndefu zitaathiri baadhi ya timu hasa zile ambazo zinatumia mabasi, lakini kwa Simba na Yanga haitakuwa ishu kwani zenyewe hutumia usafiri wa ndege na hata kama wangekuwa wanatumia mabasi sidhani kama wataruhusu uchovu wa safari kuwa kikwazo.”

Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar, Gwambina na Azam FC, Mohamed Badru alisema; “Ukiniuliza nani anachukua ubingwa naweza kuwa na wakati mgumu kukujibu kwa sababu timu zote mbili zinaonekana kuwa na nafasi kubwa kwa sababu bado wana mchezo mmoja ambao utawakutanisha, kwa mechi zilizobakia naona ubingwa ukiamuliwa kwa mchezo wao ambao haujachezwa.”

Pamoja ugumu wa dakika 720 ikiwamo kiporo cha Dabi na timu kusafiri, bado makocha wa timu zote mbili, Fadlu Davids na Miloud Hamdi watahitaji kufanya uamuzi sahihi kuhusu mzunguko wa matumizi ya wachezaji wao ili kuepuka uchovu.  

Pia makocha wa timu hizo waombe wachezaji wao nyota wasipate majeraha yanayoweza kuwapa mtihani katika hesabu hizo za ubingwa, japo ratiba za mechi zilizo na jukumu la kimataifa kwa Simba inaweza kuwapa wakati mgumu, ingawa bado kuna faida kama timu itakuwa na moto ule ule iliyonayo.

Related Posts

en English sw Swahili