Namba za JKT Tanzania zinashtua

LICHA ya kwamba hawatajwi sana, lakini maafande wa JKT Tanzania namba walizonazo katika Ligi Kuu Bara iliyosimama kwa sasa zinashtua.

Timu hiyo inayonolewa na kocha mzawa, Ahmad Ally ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 30, lakini ikishika nafasi ya nne kwa timu zilizoruhusu mabao machache 17, nyuma ya Simba (8), Yanga (9) na Azam FC (12).

Ally ndiye kocha pekee mzawa aliyepo ndani ya sita bora, kwani nyingine tano zote zinanolewa na makocha wa kigeni ikiwamo vinara Yanga, Simba iliyopo nafasi ya pili, Azam FC inayoshika nafasi ya tatu, Singida Black Stars na Tabora United iliyopo ya tano.

Chini ya Ally, maafande hao wa JKT wamecheza mechi 23 hadi sasa katika Ligi na kushinda saba, kutoka sare tisa na kupoteza saba ikiwa ni ya sita katika msimamo kwa zilizopoteza idadi ndogo ya mechi, ikiwa nyuma ya Simba iliyopoteza moja tu, Yanga (2), Azam FC (3), Singida BS (5) na Tabora Utd (6).

Kocha Ally ameiwezesha JKT kutinga robo fainali baada ya kuifumua Mbeya Kwanza katika mechi ya 16 Bora, huku timu hiyo ikifunga mabao 10 na kufungwa mawili tu hadi kufika hatua hiyo, kwani ilianza na ushindi wa 5-1 dhidi ya Igunga United katika 64 Bora, kisha kushinda 2-1 dhidi ya Biashara United katika hatua ya 32 Bora na katika 16 Bora ilishinda 2-0 kwa Mbeya Kwanza.

Rekodi zinaonyesha katika mechi 23 za Ligi Kuu, JKT imepiga jumla ya pasi 7424, na mshambuliaji, Edward Songo ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akifunga matatu, huku John Bocco akiwa na mawili sawa na aliyonayo beki wa kati, Wilson Nangu.

Hata hivyo, licha ya namba kuibeba JKT katika maeneo mengi ikiwamo katika msimamo na jinsi ya kujilinda, lakini timu hiyo ina tatizo la kufunga mabao kwani inashika nafasi ya tano kwa kuwa na idadi ndogo ya mabao nyuma ya vinara TZ Prisons (12), Pamba Jiji (14), KMC na Namungo zilizofunga 16 kila moja, kisha maafande hao sambamba na Coastal Union kila moja imefunga mabao 18.

Ili kumaliza msimu, JKT TZ sasa imesaliwa na mechi saba, ikipiga hesabu za kutaka kumaliza katika Nne Bora ili kukata tiketi ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika ikizisikilizia Azam FC, Singida BS na Tabora United zilizopo juu yake zikipambana kumaliza katika nafsi ya kucheza CAF.

Timu inayoshika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu na Bingwa wa Kombe la Shirikisho huwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika, huku mbili zilizoshika nafasi za juu akiwamo bingwa zitacheza Ligi ya Mabingwa Afrika na iwapo bingwa wa Ligi au mshindi wa pili ndiye bingwa Kombe la Shirikisho basi hutoa nafasi kwa timu iliyoshika nafasi ya nne kuungana na timu nyingine tatu kucheza CAF.

Related Posts