Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mwanaume mmoja (26), mkazi wa kijiji cha Kirwa, Wilaya ya Rombo, kwa tuhuma za mauaji ya mtoto Rosemary Mathias (06), mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mahaheni.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, tukio hilo lilitokea Machi 15, 2025, majira ya saa tisa jioni, baada ya mtuhumiwa kumkuta binti huyo akicheza na wenzake na kisha kumkata shingoni kwa kitu chenye ncha kali, na kutenganisha kiwiliwili na kichwa chake.
Mashuhuda wa tukio walisema kuwa siku hiyo, mtuhumiwa alirejea nyumbani kwake akitokea matembezini, akiwa na panga mkononi, kisha aliwashangaza watoto waliokuwa wakicheza kwa kumshika Rosemary na kutekeleza kitendo hicho cha kinyama.
Polisi wamesema uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo cha tukio hilo. Baada ya uchunguzi kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma, Wilaya ya Rombo, kusubiri uchunguzi wa kitabibu na taratibu nyingine za mazishi.