SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi Boubou Traore kutoka Mali kusimamia mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kati ya wenyeji Al Masry ya Misri na wawakilishi pekee wa Tanzania, Simba.
Traore aliyezaliwa Machi 3, 1989, amepangwa kuchezesha mchezo huo utakaopigwa Aprili 2, kwenye Uwanja wa New Suez Canal huko Misri, huku rekodi za mwamuzi huyo zikionyesha Simba inapaswa kucheza kwa tahadhari ili kupata ushindi ugenini.
Rekodi zinaonyesha mwamuzi huyo amechezesha michezo 25 ya kimataifa ambapo timu mwenyeji imeshinda 17 na zile za ugenini zimeshinda mara sita, huku mechi mbili zikimalizika kwa sare, akitoa pia jumla ya kadi za njano 86 na kadi nyekundu nne.
Mwamuzi huyo ndiye aliyechezesha mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Yanga iliyoifumua CR Belouizdad ya Algeria mabao 4-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 24, 2024 na kutinga robo fainali kibabe.
Huu utakuwa ni mchezo wa nne kwa mwamuzi huyo kuichezesha Al Masry katika michuano ya kimataifa ambapo mechi zote tatu zilizopita amekuwa na bahati na miamba hiyo, kutokana na rekodi kuonyesha imeshinda yote na kuzidi kuongeza ugumu zaidi.
Mchezo wa kwanza kwa Traore kuichezesha Al Masry ulikuwa wa ushindi wa kikosi hicho wa mabao 3-2, ugenini dhidi ya FC Nouadhibou ya Mauritania, katika Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi (kundi A), mechi ikipigwa Des Mosi, 2019.
Mechi nyingine ambayo Traore aliichezesha Al Masry, ilikuwa pia ya ushindi wa mabao 2-1, nyumbani dhidi ya RS Berkane ya Morocco, katika Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya kwanza ya robo fainali, mchezo uliofanyika Apr17, 2022.
Traore akaendeleza upepo wa bahati kwa miamba hiyo baada ya kuchezesha mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi (kundi D), ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Al Masry ikiwa nyumbani iliitandika Enyimba ya Nigeria mabao 2-0, Novemba 27, 2024.
Simba iliyomaliza kinara wa kundi A na pointi 13, imepangiwa na Al Masry iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kundi D na pointi tisa, nyuma ya wapinzani wao kutoka Misri, Zamalek ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo 2023-2024.
Kitendo cha Al Masry kumaliza nafasi ya pili huku Simba ikimaliza ya kwanza, kimezifanya timu hizo kukutana tena ambapo pambano hilo la Aprili 2, litakuwa ni la tatu kwao kukutana kwa miaka ya hivi karibuni baada ya kutokea pia mwaka 2018.
Timu hizo zilikutana raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mechi ya jijini Dar es Salaam zilitoka sare ya mabao 2-2, Machi 7, 2018, kisha marudiano Misri zikatoka suluhu (0-0), Machi 17, 2018, na Simba kutolewa kwa mabao ya ugenini.
Simba imetinga hatua ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu mwaka 2018, zikiwamo mbili ya Shirikisho Afrika na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa kinara wa kundi kwa mara yake ya pili.
Mara ya kwanza Simba kuongoza kundi tangu kipindi hicho ilikuwa msimu wa 2020-2021, iliposhiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kumaliza kinara wa kundi A kwa pointi 13, ikifuatiwa na Al Ahly ya Misri iliyomaliza ya pili kwa pointi 11.
AS Vita Club ya DR Congo ilimaliza ya tatu (pointi 7), huku Al Merrikh ya Sudan ikiburuza mkiani na pointi mbili tu, ambapo msimu huo Simba iliishia robo fainali baada ya kutolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 4-3.