UNAWEZA kusema mshambuliaji wa JKT Queens, Stumai Abdallah amepania kwenye mbio za kuchukua kiatu cha ufungaji bora Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).
Mbali na chama lake kuwania nafasi ya ubingwa ambayo hadi sasa inatetewa na Simba Queens lakini nyota huyo anaongeza ushindani mwingine kwa upande wa kiatu.
Ndio kinara wa ufungaji hadi sasa akiwa na mabao 21 nyuma ya Jentrix Shikangwa mwenye nayo 17 kwenye raundi 12 za WPL.
Nyota huyo wa timu ya taifa ‘Twiga Stars’ amekuwa na mwendelezo wa ufungaji kwa takribani misimu mitano mfululizo lakini ni kama hakuwa na bahati ya kiatu akishuhudia kikienda kwa nyota wengine.
Sasa msimu huu kama atakuwa na muendelezo huo huenda akachukua kiatu cha dhahabu ambacho pia kinatolewa macho na Shikangwa mwenye mabao 17.
Katika mchezo uliopigwa Machi 12 dhidi ya Gets Program, Stumai alifunga mabao matatu na kumfanya afikishe jumla ya hat-trick nne kwenye ligi akiwa kinara.