WAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na rasilimali zao licha ya uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili kumpa onyo juu ya kutokana na malalamiko ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi kuwa alitoa kauli za kichochezi, zisizo na staha na zisizozingatia taaluma ya uwakili. Anaripoti Faki Sosi… (endelea).
Mwabukusi amepewa onyo baada ya Julai mwaka jana, Dk. Feleshi kupeleka shauri lake katika kamati hiyo akilalamika juu ya kauli alizozitoa Mwabukusi wakati akizungumza na vyombo vya habari.
Moja ya kauli iliyotajwa katika malalamiko hayo ni maneno ya Mwabukusi kwamba, “Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hawajui walichopitisha Bungeni kwamba hata Chifu Mangungo anasingiziwa maana yeye alijua ni Mkataba.”
Wakili Mwabukusi alikuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Mkataba kati ya Tanzania na Dubai, mkataba unaoipa kampuni ya DP World ya Dubai kuendesha, kuboresha na kuendeleza bandari za Tanzania.
Aidha, akizunguma na waandishi wa habari jana Ijumaa Mwabukusi alisema kuwa hatokubali kufungwa mdomo ilhali sheria na Katiba ya nchi zinampa wajibu wa kutetea rasilimali za nchi.
Mwabukusi amesema kuwa amegundua udhaifu kwenye mifumo ya sheria ambayo inawataka mawakili kukaa kimya kisa maadili ya uwakili wakati ni jukumu la kila Mtanzania kulinda na kutetea pale ambapo anapoona haki za nchi na wananchi wengine zinapokwa.
“Ni lazima mawakili, wanaharakati wanaopenda kutetea haki za kijamii kwanza waelewe ni shughuli ngumu ni shughuli zisizokuwa na pesa… ni shughuli ambazo mara nyingi serikali hupenda kuzidhibiti kwa kutumia nguvu kubwa.
“Licha ya changamoto tunazozipitia, licha ya kashkash hatutakiwi kuogopa, hatutakiwi kurudi nyuma, hatutakiwi kufungwa midomo… sisi tunawajibu mkubwa zaidi kuliko Watanzania wenzetu.
“Haiwezekani sheria zinakiukwa mtu akuambie tu uende mahakamani usiongee lazima tuwaambie Watanzania sheria imekiukwa kwa namna gani, makosa gani yanafanyika, kwanini yanafanyika, nini wafanye wao kama Watanzania,” alisema Mwabukusi.
Mwabukusi alisema kuwa anatamani kuona sheria inayotumia nguvu kubwa kuwafunga midomo mawakili ingetumika kuwawajibisha wahalifu.
“Mawakili wenzengu tujue tuna kazi kubwa, tuhakikishe sheria zetu zinatoa mwangaza, ukiona sheria zetu zinatumia nguvu kubwa kuwafunga midomo mawakili, nguvu hiyo haitumiki kuwaadhibu wahalifu basi ujue kuna tatizo,” aliongeza.
Alisema kuwa hatokubali kuzibwa mdomo licha ya vitisho vilivyomkabili wakati akizungumzia suala la haki za watanganyika na ataendelea kuzungumza kwa uzito wake.
“Nikizungumza juu ya ulinzi wa rasilimali za watanganyika nitazungumza kwa uzito wake, nikizungumza suala la utawala bora na demokrasia nitazungumza kwa uzito wake na wote wajue kwamba tupo tayari kulipa ghrama, niwape moyo watetezi, tusikate tamaa, tusifungwe na hivi vitisho,” alisema na kuongeza;
“Hatua niliyopitia nimeona madhaifu nimeona tatizo lilikuwepo la kisheria, ninarudi mahakama kuondoa hilo tatizo lakini nina kwenda kwenye jamii kupeleka uhamasishaji, sitakubali kunyamaza na kuicha jamii yangu ikiendelea kudanganywa. Watu wanazunguka wanasema uongo wa dhahiri halafu wanataka tusiwajibu wao ni nani ni miungu, hii nchi inaongozwa kwa mujibu wa sheria na Katiba,” alisema Mwabukusi.
Mwabukusi alitoa wito kwa wanasheria kuzifahamu nyema sheria za nchi ili kuwa chachu ya mageuzi nchini.
“Uwakili sio kuvaa majoho na kwenda mahakamani halafu unatoka unakaa kimya kama bubu halafu watu wanapotosha na wanaharibu nje.. hapana! haki yetu tunawajibu wa kuulinda katiba huwezi kuchukua haki yangu ya kiraia kisa uwakili, chukua uwakili nibaki na haki yangu ya kiraia, nibaki kuwa raia mwaminifu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Mtanganyika halisi.
“Sheria na Katiba zinalindwa na wananchi, nchi inapovamiwa tunaposema kuvamiwa kwa nchi maana yake hata mikataba ya kizembe inayouza ardhi na rasilimali za nchi ni kuvamiwa kwa nchi,” alisema.
Aidha, Mwabukusi alisema bado hajapewa nakala ya uamuzi huo na kwamba akishapewa na kuusoma wote atajitokeza hadharani na kueleza hatua zaidi na kama uamuzi huo utachukua haki yake ya utetezi wa rasilimali hatokubali atapiga hatua zaidi kuisaka haki yake.