WADAU WAIANGUKIA SERIKALI KURIDHIA MKATABA WA MASUALA YA WATU WENYE ULEMAVU AFRIKA

Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu,Wakili Gideon Mandes, alizungumza na waandishi wa habari mara baada ya semina ya Waandishi wa habari na wadau kutoka vyama vya watu wenye ulemavu yaliyoandaliwa na Shirika la Sightsavers yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa itifaki hiyo.

Na.Mwandishi Wetu

KATIKA kukabiliana na mila, imani potofu na ushirikina unaodhuru watu wenye ulemavu, wadau wameiangukia serikali kukamilisha mchakato wa kuridhia Itifaki ya masuala ya watu wenye ulemavu Afrika kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la 12 ili kulinda haki zao.

Itifaki hiyo inatokana na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu uliopitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika katika Mkutano wa 30 wa kawaida wa Bunge mnamo Januari 2018 na hadi sasa Tanzania bado haijaridhia.

Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dodoma na wadau kutoka vyama vya watu wenye ulemavu na waandishi wa habari katika mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Sightsavers yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa itifaki hiyo.

Akizungumza kuhusu faida za itifaki hiyo, Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu,Wakili Gideon Mandes, alisema katika mkataba huo kuna haki za watu wenye ulemavu katika masuala ya elimu, ajira, afya, fursa za kiuchumi na miundombinu inayofikika.

Pia, alisema mkataba huo unaongelea masuala ya uwakilishi wa watu wenye ulemavu katika shughuli za kisiasa na umma, haki za wanawake, wasichana na watoto.

“Tanzania bado hatujaridhia kwasababu moja kwanza ilitakiwa mchakato upitie serikalini na serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar tupate maoni ili kwenda kwenye hatua nyingine za michakato ya itifaki,”alisema.

Naye, Mjumbe wa Shirikisho la Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) Dodoma, Sophia Mhando, alisema wanawake wenye ulemavu wanaomba serikali iridhie mkataba huo ili kuweka uchechemzi wa haki zao za kiafya kwenye sera na sheria zinazotungwa.

Mratibu wa mradi wa macho wa Shirika la Sightsavers, Upendo Minja, alisema shirika hilo limetambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa hamasa kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu zinalindwa na mkataba huo kuridhiwa.

Alisema hadi sasa nchi 16 zimeridhia na kwa kupitia vyombo vya habari wananchi watajua umuhimu wa mkataba huo kwa Tanzania na kuhamasisha serikali kuridhia mkataba huo.

Awali, Ofisa wa Sera, uchechemuzi na ushawishi Kanda ya Afrika Mashariki Kati na Kusini wa Sightsavers, Neema Kalole, alisema ni muhimu kwa Tanzania kuridhia mkataba huo ambao unakwenda kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu kwa Afrika zinalindwa kwa kuwa kuna mambo hayafanani na nchi zingine zilizoendelea.

“Mfano mauaji ya watu wenye ulemavu wa Ngozi (albino) ni kitu ambacho kinatokea kwenye nchi zetu za Afrika na mkataba huu utaenda kuongelea kinagaubaga mazingira yaliyopo kwenye nchi zetu yatatuliwe, mkataba huu una manufaa mengi sana,”alisema.

Alisema mkataba huo unaendana na jitihada zinazofanywa na serikali za kuweka kipaumbele kutetea haki za watu wenye ulemavu na kwamba tayari kuna mapitio ya Sera ya Mwaka 2004 ambayo yanachochea utetezi huo na mkataba huo ukiridhiwa utaongeza nguvu na Tanzania itaonesha namna ilivyojizatiti kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za watu wenye ulemavu.

Related Posts