Chato. Mamia ya wananchi wa ndani na nje ya Wilaya ya Chato mkoani Geita wameungana na familia ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli katika misa takatifu ya kumuombea.
Magufuli alifikwa na mauti Jumatano ya Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.
Leo Jumatatu, Machi 17, 2025 ni miaka minne imetimia na kunafanyika misa ya kumwombea inayofanyikia katika Parokia ya Mtakatifu Yohana Muzey, Chato.

Mjane wa Magufuli, Mama Janeth pamoja na familia ni miongoni mwa waliojitokeza kanisani hapo kwenye misa hiyo inayoongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi.
Miongoni mwa viongozi walioungana na familia ni mawaziri, William Lukuvi (Sera, Bunge na Uratibu) na Innocent Bashungwa (Mambo ya Ndani). Mbunge wa Chato, Dk Merdad Kaleman naye yupo.
Wengine ni, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Jumuiya ya Vijana wa chama hicho (UVCCM).
Jana Jumapili, Machi 16, 2025, wananchi, viongozi na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) waliungana na familia kwenye matembezi ya amani kuenzi juhudi zake wakati wa uhai wake.

Katika matembezi haya yaliyo ratibiwa na familia kwa kushirikiana na UVCCM yamewahusisha watu mbalimbali ikiwemo baadhi ya viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo ambao walifika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) na kutoa mkono wa pole kwa wagonjwa waliolazwa kama sehemu ya matendo ya huruma kwa wahitaji.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Magufuli, mtoto wa marehemu, Jesca alisema familia hiyo inaungana na Watanzania wote kuelekea kumbukizi ya kifo cha mzazi wao kwa kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa.

Jesca alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuendeleza mema yote yaliyoachwa na mtangulizi wake ambapo, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato ni moja ya mradi ambao Rais Samia aliahidi kuuendeleza toka kwa Magufuli na sasa hospitali hiyo imekuwa mkombozi wa wananchi wa Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi