Mbeya City yaweka rekodi Shirikisho

MBEYA City imekuwa ni timu ya kwanza ya Ligi ya Championship kuweka rekodi ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) msimu huu, baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Machi 13 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Msimu huu ni timu sita pekee zilizofuzu 16 bora ikiwa ni rekodi, kwani msimu uliopita wa 2023-2024, hakuna klabu yoyote iliyoshiriki Ligi ya Championship iliyofika hatua hiyo na zote 16 ziliishia hatua ya 64 na 32 bora tu.

Mbeya City sasa imeifikia rekodi ya msimu wa 2021-2022 ya Pamba Jiji iliyopo Ligi Kuu na ndiyo ilikuwa timu pekee ya Championship iliyofika robo fainali ya FA na kufungwa na Simba mabao 4-0.

Msimu wa 2022-2023, timu nne zilizofuzu 16 bora ni JKT Tanzania (kwa sasa Ligi Kuu), Green Warriors, African Sports na Pan Africans, huku msimu huu ni sita ambazo ni Mbeya City, Mtibwa Sugar, Mbeya Kwanza, Stand United, Bigman FC na Songea United.

Sahare All Stars ya Tanga ndiyo inayoshikilia rekodi ya timu za Championship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo msimu wa 2020-2021, japo ilitolewa na ‘Wauaji wa Kusini’ Namungo kwa kufungwa bao 1-0.

Mtibwa inaungana na Mbeya Kwanza iliyochapwa 3-0 na JKT Tanzania, hivyo kubakia timu nne tu za Stand United itakayocheza na Giraffe Academy, Bigman FC ikicheza na Simba, huku Songea United ikiivaa Yanga katika mechi za hatua ya 16 bora zitakazochezwa mwishoni mwa mwezi huu.

Kwa mujibu wa ratiba ya mechi hizo zilizosalia ni Machi 26, Stand United na Girrafe zitamalizana mjini Shinyanga, huku Simba itavaana na Bigman siku inafuata na Machi 28 itakuwa zamu ya Tabora United kuvaana na Kagera Sugar na Machi 29, zitapigwa mechi mbili, Yanga na Songea United na Mashujaa itatunishiana misuli na Pamba Jiji, mjini Kigoma, ili kutinga robo fainali.

Related Posts