Gachagua anavyozidi kumkaba koo Rais Ruto

Nairobi. Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ameendelea kuikosoa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto, akiwataka wakazi wa Mlima Kenya kujiandaa kuunda chama kipya ifikapo Mei mwaka huu. 

Akizungumza kwa njia ya simu Jumamosi Machi 15, 2025 wakati wa mazishi ya vijana watatu waliopoteza maisha kwenye ajali ya barabarani katika Kijiji cha Kinyakiiru, Kaunti ya Kirinyaga, Gachagua amesema UDA imekuwa chanzo cha mateso kwa watu wa eneo hilo. 

“UDA ni nyumba iliyojaa matatizo. Chama hiki kinaendeshwa kwa misingi ya uwongo na ndiyo maana miradi ya barabara imesimama, wanafunzi wa vyuo vikuu wamekwama nyumbani kwa kukosa karo, na bima mpya ya afya ya jamii (SHIF) haifanyi kazi,” amesema Gachagua, huku waombolezaji wakimshangilia. 

Amesema Mlima Kenya ilifanya kosa kushiriki uchaguzi mkuu wa 2022 bila chama chao mahsusi na akaonya wasirudie kosa hilo tena. 

“Lazima tujifunze kutokana na makosa yetu. Tusiruhusu historia kujirudia mwaka 2027,” amesisitiza. 

Mbunge huyo wa zamani wa Mathira pia amewatupia lawama wabunge wa Mlima Kenya waliounga mkono hoja ya kumvua wadhifa wake wa Naibu Rais, akisema wataadhibiwa na wapigakura. 

Seneta wa Kirinyaga Kamau Murango, Mwakilishi wa Kaunti hiyo Njeri Maina, na Diwani wa Baragwi, David Mathenge walimuunga mkono Gachagua, wakisema hawataruhusu wakazi wa Mlima Kenya kudhulumiwa tena. 

Alivyondolewa madarakani 

Rigathi Gachagua aliondolewa kwenye nafasi ya Naibu Rais baada ya mvutano wa muda mrefu kati yake na Rais William Ruto.

Utofauti wao ulianza kuonekana hadharani baada ya Gachagua kuanza kushinikiza maslahi ya Mlima Kenya, akidai kuwa eneo hilo lilikuwa limeachwa nyuma katika ugavi wa rasilimali na uteuzi wa viongozi serikalini. 

Mvutano huo ulifikia kilele pale ambapo baadhi ya wabunge wa UDA kutoka Mlima Kenya walijiunga na kambi ya Rais Ruto na kuunga mkono mchakato wa kumvua madaraka Gachagua. Hatua hiyo ilimfanya kupoteza nafasi yake, hali iliyozua mgawanyiko mkubwa kisiasa katika eneo hilo. 

Rais William Ruto alieleza kuwa alimuondoa Gachagua, kutokana na kueneza chuki, ukabila, na migawanyiko miongoni mwa Wakenya.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la Kondele, Kisumu, Novemba 2024, Ruto alisema hatavumilia viongozi wanaoendeleza maovu hayo na kwamba tayari amewaondoa wale waliohusika na vitendo hivyo.

Gachagua alitimuliwa na Bunge la Seneti mwezi Oktoba kwa mashtaka ya ukiukaji mkubwa wa katiba na uchochezi wa chuki za kikabila, madai ambayo aliyakana akiyaita ya kisiasa.

Baada ya kuondolewa, alilalamika kuwa ulinzi wake umeondolewa na kwamba maisha yake yako hatarini, akimshutumu Rais Ruto kwa ukatili dhidi yake.

Vilevile Gachagua amekuwa akitoa matamko mbalimbali tangu aondolewe madarakani ikiwemo ya kudai kuwa baadhi ya wasaidizi wa Rais wanamhujumu kutokana na msimamo wake wa kusema ukweli, akisisitiza kuwa uaminifu wake kwa wananchi umemletea upinzani ndani ya serikali.

Aidha, Gachagua amewahi kujitokeza hadharani akipinga uwezekano wa ushirikiano kati ya serikali na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, kupitia makubaliano ya “handshake”.

Ikumbukwe Rais Ruto alimteua Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, kuchukua nafasi ya Gachagua kama Naibu Rais mpya.

Hata hivyo, mchakato wa kumuapisha Kindiki ulisitishwa kwa muda na Mahakama Kuu baada ya Gachagua kuwasilisha rufaa kupinga kuondolewa kwake.

Kwa sasa, Gachagua anapanga kuanzisha chama kipya ambacho amesema kitakuwa sauti ya kweli ya watu wa Mlima Kenya katika siasa za Kenya kuelekea uchaguzi wa 2027.

Related Posts