Hatma vita ya Ukraine kujulikana kesho

Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump amesema atazungumza na Rais wa Russia, Vladimir Putin kesho Jumanne Machi 18, 2025, kuhusu hatima vita ya Russia na Ukraine.

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti leo Jumatatu Machi 17, 2025, kuwa kiongozi huyo wa Marekani alifichua jana Jumapili kuhusu mazungumzo hayo yajayo alipokuwa akisafiri kutoka Florida kwenda Washington DC kwa ndege maalumu ya Air Force One.

“Tutaona kama tutakuwa na kitu cha kutangaza labda ifikapo Jumanne. Nitazungumza na Rais Putin Jumanne. Kazi nyingi zimefanywa mwishoni mwa wiki. Tunataka kuona kama tunaweza kumaliza vita hivyo,” amesema Trump.

Mazungumzo yoyote kama hayo yanaweza kuwa hatua muhimu katika mzozo huo na fursa kwa Trump kuendelea kuimarisha upya Sera ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Washirika wa Ulaya wana hofu kuhusu uhusiano wa Trump na Putin na msimamo wake mkali dhidi ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, ambaye alikabiliwa na ukosoaji mkali alipokwenda Ikulu ya Marekani zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Hata hivyo, Russia imeendelea kuyatwaa maeneo makubwa ya Ukraine tangu ilipotangaza Operesheni yake ya kijeshi Februari 2022, ambapo hadi sasa imeyatwaa maeneo ya Mkoa wa Donetsk, Luhansk, Kherson, Pokrovisk na Crimea iliyotwaliwa kutoka Ukraine tangu 2014.

Pia, Rais Putin alitangaza wiki iliyopita kuwa sehemu kubwa ya Mkoa wa Kursk ambao ulikuwa unakaliwa na vikosi vya Ukraine imerejeshwa mikononi mwake na vikosi vya Russia huku akikubaliana na pendekezo la kusitishwa kwa mapigano hayo kwa siku 30.

Katika maelezo yake ya jana Trump alisema ardhi ya Ukraine iliyoko mikononi mwa Russia na mitambo ya uzalishaji wa nishati ikiwemo umeme ni sehemu ya mazungumzo kuhusu kumaliza vita hivyo.

“Tutazungumza kuhusu ardhi. Tutazungumza kuhusu mitambo ya umeme. Tutagawanya mali fulani,” amesema Trump.

Mjumbe maalum wa Trump kwenye mzozo huo, Steve Witkoff, hivi karibuni alitembelea Russia kuendeleza mazungumzo huku akisema mapema Jumapili kuwa simu kati ya Trump na Putin ingeweza kufanyika hivi karibuni.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts