Tanzania imekuwa mwenyeji wa Warsha ya siku tano ya Mfumo wa Uboreshaji wa Usafiri wa Anga (ASBU) 2025 inayofanyika Jijini Dar es Salaam.
Warsha hiyo inayofanyika katika Hoteli ya Ramada, imefunguliwa rasmi Machi 17 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw.Salim Msangi.
Lengo la wadau hawa kukutana ni kujadili na kuimarisha mikakati ya kuboresha usalama wa anga, ufanisi wa usambazaji, na uendelevu wa sekta hiyo kwa kuzingatia teknolojia za kisasa na miongozo ya kimataifa.
Kwa upande Bw.Sylvestre Sinarinzi, Afisa Mkuu wa Huduma za Usambazaji wa Anga (ANS) katika Shirika la Usimamizi wa Usalama wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CASSOA), alitoa shukrani kwa Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa warsha hiyo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika maendeleo ya sekta ya anga.
“CASSOA imejitolea kushirikiana na wadau wote muhimu ili kuhakikisha kuna mafanikio makubwa katika sekta ya anga. Tunaamini kuwa kwa kushirikiana, tunaweza kuimarisha usalama na ufanisi wa urambazaji wa anga katika kanda yetu,” alisema Sinarinzi.
Akitoa maoni yake mmoja wa washiriki wa warsha hiyo Bi. Enia Kakombu kutoka Zambia, ambaye alielezea furaha yake ya kushiriki na kujifunza kutoka kwa wataalamu mbalimbali wa sekta ya anga.
“Nina furaha kubwa kuwa sehemu ya warsha hii. Nimejipanga kujifunza na kushirikiana na wengine ili kuhakikisha tunafanikisha malengo ya warsha hii,” alisema Kakombu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi akizungumza
na wadau mbalimbali wa sekta ya anga kutoka zaidi ya nchi 13 za Afrika wakati wa ufunguzi wa warsha ya Mfumo wa Uboreshaji wa Usafiri wa Anga (ASBU) 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Afisa Mkuu wa Huduma za Urambazaji wa Anga (ANS) katika Shirika la Usimamizi wa Usalama wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CASSOA) Sylvestre Sinarinzi akitoa shukrani kwa Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa warsha hiyo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika maendeleo ya sekta ya anga wakati wa ufunguzi wa Mfumo wa Uboreshaji wa Usafiri wa Anga (ASBU) 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau mbalimbali wa sekta ya anga kutoka zaidi ya nchi 13 za Afrika, zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Angola, Mauritius, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Zambia, na Namibia wakiwa kwenye ufunguzi wa warsha ya Mfumo wa Uboreshaji wa Usafiri wa Anga (ASBU) 2025 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja