Rais Samia azindua mfumo utakaondoa kumilikishwa kiwanja kimoja watu wawili

Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua mfumo wa kidijitali wa kutoa hati kwa kidijitali unaofahamika kama E-Ardhi utakaomaliza tatizo la watu wawili kumilikishwa kiwanja kimoja.

Rais Samia amezidua mfumo huo leo Jumatatu Machi 17, 2025 wakati wa halfla ya uzinduzi wa sera ya Ardhi ya mwaka 1975 toleo la mwaka 2023.

Akielezea mfumo unavyofanya kazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi amesema awali hati zilihifadhiwa kama karatasi na kujaza masijala.

Kuna wakati, amesema karatasi hizo zilikuwa zikipotea na kuleta migogoro ya kupewa hati mara mbili, lakini mfumo wa E-ardhi utalikomesha hilo.

Amesema mfumo huo unasomana na mifumo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Amesema mfumo huo unatumika katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Arusha na uko katika hatua za mwisho kukamilika na kuanza kutumika mkoani Mbeya.

Ndejembi amesema hadi kufikia mwaka 2027 watakuwa wamekamilisha mchakato wa kutumia mfumo huo nchi zima kwa kuwa kuhakikisha nyaraka zote zinaingia katika mfumo huo zinachukua muda.

Ndejembi amesema Tanzania kwa mara ya mwisho ilikuwa na ramani iliyoonyesha kila kitu kilichoko mwaka 1978 na kwa kuwa miji imekuwa na mingine imeongezeka itapatikana mpya.

“Lakini kama nchi bado tulikuwa tunatumia ramani ya mwaka 1978, kuna vingine ambavyo havipo sasa vilivyokuwepo katika mwaka huo, kuna misitu ambayo ilikuwepo lakini hivi sasa haipo tena, kwa hiyo kwa kutupatia zaidi ya Sh173 bilioni tunaenda kuipima (scan) nchi nzima kidijitali na kuweza kuwa na ramani moja,” amesema.

Ndejembi amesema ramani hiyo itatumika na taasisi zote za kiserikali na sekta binafsi kwa maaana kama ni Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ama Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) wataona kilichoko.

Amesema katika mchakato huo, watatumia setilite, ndege zisizokuwa na rubani na ndege ambayo itapita nchi nzima kupima.

Ndejembi amesema ukuaji wa miji umekuwa mkubwa tofauti na mwaka 1970 ukuaji ulikuwa ni wa asilimia 5.7  na hivyo kusababisha ukuaji holela wa makazi na kuwa wanao mpango wa kufanya maendelezo upya.

Amesema mpango huo utafanyika Majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya na kuwa baada ya kutoa maelekezo ya Rais Samia katika eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam walijifunza kitu.

Amesema kwa kufanya ushirikishwaji na wananchi wenyewe lakini kuna maeneo mengine watashirikiana na sekta binafsi katika kuyaendeleza upya maeneo hayo ambayo yamejengwa kiholela.

Amesema wameshakagua kaya zaidi ya 5,000 ili kuona ni jinsi gani watafanya katika kuyafanya makazi ya kisasa na yenye thamani kuliko ilivyo hivi sasa.

Akijibu swali la Rais Samia kuwa wakazi waliopo watakwenda wapi wakati wanafanya shughuli hiyo, Ndejembi amesema wakazi hao watatafutiwa makazi mengine na utakapokamilika watarejea tena katika makazi hayo, huku eneo litakalobaki litatumika kwa ajili ya shughuli nyingine za kiserikali.

Endelea kufuatilia Mwananchi kinachoendelea kwenye hafla hiyo.

Related Posts