Kumbukumbu sita kubwa za Magufuli michezoni

Hayati Magufuli alifariki Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo, kifo kilichohitimisha miaka mitano ya utawala wake.

Yapo ambayo wanamichezo wanayakumbuka kwa hayati Magufuli ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza Novemba 05, 2015 na leo hii inapotimia miaka minne mwili wake ukiwa ardhini, yanabakia katika historia.

Ahadi ya ujenzi Uwanja wa soka Dodoma

Oktoba 24, 2016 Rais Magufuli alitoa ahadi ya kujenga Uwanja wa mkubwa wa soka mkoani Dodoma ambao ungeingiza idadi ya mashabiki 80,000.

Hayati Magufuli alisema kuwa Uwanja wa huo utajengwa kwa ufadhili wa serikali ya Morocco chini ya Mfalme Mohammed VI na ungegharimu kiasi cha Dola 100 milioni (Sh266 bilioni).

Hata hivyo hadi anafariki, ahadi hiyo haikutimia lakini kwa sasa, serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imepanga kujenga Uwanja wa kisasa mkoani Dodoma ambao utaingza mashabiki 32,000 kwa gharama ya Sh350 bilioni, fedha ambazo zote zitalipwa na serikali.

Taifa Stars kupewa viwanja

Machi 25, 2019, hayati Rais Magufuli alitoa zawadi ya viwanja mkoani Dodoma kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ baada ya timu hiyo kufanikiwa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon)  ambazo mwaka huo zilifanyika Misri.

Taifa Stars ilifuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L la kuwania kufuzu ikiwa na pointi nane huku kinara Uganda ikimaliza na pointi 13.

Rais Magufuli alitoa ahadi ya viwanja pia kwa wachezaji wawili wa zamani wa Taifa Stars ambao waliiongoza timu hiyo kufuzu Afcon 1980 ambao ni Leodgar Tenga na Peter Tino.

Bondia Hassan Mwakinyo naye alipewa zawadi ya kiwanja kwa  kumshinda kwa Knockout (KO) raundi ya tano Muargentina, Sergio Eduardo Gonzalez katika pambano lililofanyika siku tatu kabla huko Nairobi, Kenya.

Kuhudhuria ‘Kariakoo Derby

Machi 09, 2020, iliandikwa historia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya Rais John Magufuli kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda uwanjani kutazama mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba ‘Kariakoo Derby’.

Katika mchezo huo, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililopachikwa na Bernard Morrison.

Sh1 bilioni Serengeti Boys

Katika kufanikisha maandalizi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwa ajili ya ushiriki wa fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo zilizofanyika nchini, mwaka 2019, Machi 25, 2019, Rais Magufuli alitoa kiasi cha Sh 1 bilioni kwenda Wizara inayohusika na michezo.

“Nikimwaga hela (fedha) hapa na nyinyi lazima mkamwage magoli ili kufikia malengo mliyoniahidi,” alisema Rais Magufuli.

Wakati wa hotuba ya ufunguzi wa Bunge la 12 jijini Dodoma, Novemba 13, 2020, Rais Magufuli aliahidi serikali kuanza kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya timu za taifa

“Tutaanza kutenga fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kuzianda timu zetu za Taifa na katika hilo napenda kutumia fursa hii, kuitakia heri timu yetu ya Taifa kwenye mechi yao dhidi ya Tunisia hapo baadaye,” alisema Magufuli.

Jina la Uwanja Benjamin Mkapa

Wakati wa shughuli ya kuaga kitaifa mwili wa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Mkapa kwa viongozi na wananchi iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Julai 28,2020, Rais Magufuli aliagiza uilokuwa ukiitwa Uwanja wa Taifa kubadilishwa jina na kuwa Benjami Mkapa kama sehemu ya kumuenzi marehemu Mkapa, aliyetoa wazo na seriokali yake kuchangia ujenzi wa uwanja huo.

“Wengi wanataka Uwanja ule uitwe Uwanja wa Mkapa, ninajua hakupenda sana vitu viitwe kwa jina lake, lakini sasa hawezi niadhibu natamka rasmi utaitwa Uwanja wa Mkapa ili tuweze kumuenzi na kumkumbuka kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa ajili ya kuendeleza maslahi ya michezo kwa taifa letu,” alisema Rais Magufuli.

Related Posts