Hizi hapa changamoto zinazokabili sekta ya maji, mwarobaini

Dar es Salaam. Mabadiliko ya tabianchi, upotevu, wizi kwa baadhi ya watu na gharama za utekelezaji wa miradi ya maji zimetajwa kuwa changamoto zinazoikabili sekta ya maji huku Wizara ikisisitiza umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji.

Aidha, upotevu wa maji wakati wa usambazaji unawezekana ukawa wa kibishara au binafsi, bomba kupasuka, changamoto hizo zinaanikwa wakati Tanzania ikitajwa kuwa na maji ya kutosha yaliyopo juu na chini ya ardhi.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kikao maalumu cha wadau wa maji kinachohusu mapitio ya sekta hiyo kilichofanyika kwenye ufunguzi wa wiki ya maji inayoanza leo Jumatatu Machi 17, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City.

“Changamoto nyingine ni gharama ya usambazaji wa maji kutoka kwenye vyanzo kwenda maeneo mbalimbali yasiyo na maji kuyatibu, mchakato ambao unahitaji fedha nyingi,” amesema.

Amesema kulingana na hali hiyo Wizara inaendelea kukabiliana na changamoto huku ikisisitiza kutunza vyanzo vya maji kutokana na athari zitokananazo na mabadiliko yatabianchi.

Amesema ndio maana Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya athari hizo.

“Huduma ya maji inaendelea kuimarika ila changamoto inayotukabili ni mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri vyanzo vya maji ambayo si Tanzania tu hata mataifa mengine. Hata hivyo, bado hatujafikia kwenye ukosefu wa maji,” amesema Katibu huyo Mkuu.

Akizungumzia hali ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa sasa uliopo nchini hivi sasa kwa maeneo ya vijijini imefikia asilimia 83 kutoka 79 mwaka 2020 huku mijini imefikia asilimia 91.6 kutoka asilimia 84 mwaka 2020.

“Lengo letu ni kufikia asilimia 85 vijijini na 95 mijini. Maendeleo haya yanatokana na mradi wa maendeleo ya maji unaoshirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema maji yaliyopo juu na chini ya ardhi yapo ya kutosha kuhudumia mtu mmojammoja juhudi zilizopo ni kuyatafuta ya chini na kuyasambaza ya juu ili yaweze kutumiwa.

Katika kukabiliana na hali hiyo amesisitiza utunzwaji wa vyanzo vya maji ili viweze kututunza ili maji yapatikane yaweze kusambazwa.

Amesema wadau wa maendeleo wanasisitiza kuangalia ubora wa maji unaopatikana na maabara zilizopo pamoja na kuangalia namna gani huduma hiyo inapatikana kwa wananchi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said, amesema hadi kufikia mwaka 2030 lengo ni kuwa na maji kwa asilimia zote hivyo sekta hiyo inapewa kipaumbele kwani inakuza uchumi wa nchi.

Amesema kikao hiko kinakutanisha wadau wasekta wa maji kutazama tathimini ya uwekezaji sekta ya maji kuanzia usambazaji na upatikanaji.

“Mradi wa maendeleo ya sekta ya maji ulioanza mwaka 2006 hadi 2026 unahakikisha yanamfikia kila mwananchi kama ilivyo kwenye dira yetu ya maendeleo,” amesema.

Amesisitiza kutunza vyanzo vya maji kama kauli mbiu inavyosema ‘Lazima tutunze vyanzo vya maji kwaajili ya usalama wa maji yetu.’ Huku akisema suala hili linamgusa kila mtu.

Related Posts