Tanga. Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga, wameishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka bei rafiki ya kubadilisha mitungi ya gesi ya kupikia itakayosaidia hata wenye kipato kidogo kuimudu.
Wakizungumza kwenye hafla ya kugawa majiko banifu na mitungi ya gesi kwa wananchi wa eneo hilo iliyofadhiliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini(Rea) na Taifa Gas leo Mei 18,2024, wakazi hao wamesema hilo litasaidia kufanikisha kampeni ya kutunza mazingira ikiwamo uhamasishaji matumizi ya nishati safi.
Mkazi wa Msomera Joshua Laizer amesema Serikali lazima iangalie utaratibu wa kuweza kupunguziwa bei ya kubadilisha mitungi ya gesi ya kupikia kwa kuwa Sh23,000 baadhi ya wananchi hawaimudu, hivyo ipo hatari ya majiko hayo kwenda kuwekwa ndani.
Amesema kwa maisha ya kawaida wapo wananchi wanashindwa hata kununua umeme wa Sh2,000,hivyo mzigo wa Sh23,000 bado ni mkubwa kwa baadhi ya wananchi na hilo serikali inatakiwa kukaa chini kuliangalia upya.
Aidha Maria Melau amesema kuna faida nyingi kwa wananchi kuhamasishwa kutumia majiko ya gesi, kwa kuwa wanaotumia kuni kupikia wanaumia macho.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka viongozi kuanzia ngazi ya madiwani, Serikali za vijiji na mitaa mpaka kwenye vitongoji lazima wajihusishe kwenye kampeni ya kutunza mazingira, ikiwamo kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Amesema wananchi wanatakiwa kuhamasishwa kutumia nishatisafi inayohusisha majiko hayo banifu yasiotumia mkaa mwingi au gesi, lengo likiwa kuhakikisha mazingira yanalindwa.
“Ni lazima tutunze mazingira kupitia kupikia nishati safi, majiko banifu haya yaliyotolewa na Rea yana thamani ya Sh82 milioni na ni zaidi ya Sh200 milioniĀ tunapoleta hapa, huu ni uwekezaji kwa ajili ya kutunza mazingira,” amesema Kapinga.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amewataka wananchi ambao watakosa majiko hatua za awali wasilalamike kwa kuwa mpango wa Serikali ni kugawa majiko hayo kwa wananchi wote wa Msomera.
Msando amesema Serikali ya wilaya itahakikisha inasimamia kazi ya ugawaji wa majiko hayo bila upendeleo na kwa wale wenye kaya zaidi ya moja itawabidi kununua mengine wenyewe.