Vijana wahimizwa kufuata misingi ya dini, maadili

Dar es Salaam. Ili kuwa na jamii iliyobora vijana nchini wamehimizwa kuishi kwa kufuata miongozo na misingi ya dini.

Wito huo umetolewa usiku wa Machi 17, 2025 na Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Waithna’ashariyyah Tanzania (TIC), Hemed Jalala wakati wa hafla ya uzinduzi wa tafsiri ya Qur’an ya Marhum iliyofanywa na marehemu Sheikh Hassan Mwalupa enzi za uhai wake.

Mwalupa ambaye alifariki dunia mwaka 2021 alikuwa kiongozi wa dini ambaye alitumia muda wake kufasili baadhi ya vitabu vya dini ya kiislamu ikiwemo Qur’an kutoka katika lugha ya Kiarabu kwenda Kiswahili.

Lengo lilikuwa kufanya wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili kuweza kuelewa vyema vitabu hivyo takatifu.

Akizungumza katika hafla hiyo Jalala amesema vijana wakiishi kwa kufuata dini itasaidia kuwa na kizazi chenye maadili na hofu ya Mungu.

Pia amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kutengeneza masheik na maulamaa wa baadae.

“Vitabu vya dini vimetoa miongozo kuhusu misingi ya malezi ya watoto na suala la maadili hivyo vijana wakisoma dini na kuielewa ipasavyo itasaidia kuondoa changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii,”amesema Sheikh Jalala

Vilevile amesema amewahimiza watanzania kuilinda amani, utulivu kwa mwaka huu ambapo nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2025.

Kwa upande wake ambaye ni mwakilishi kutoka tasisi ya dini ya kiislamu ya Al- Itra Hemed Lubumba amesema asilimia 75 ya Taifa la Tanzania linaundwa na vijana hivyo uwingi huo ujikite katika kuiishi misingi ya kudumisha amani kama ngao ya maendeleo endelevu.

Related Posts