Katika mtalaa mpya wa masomo katika shule za msingi tumeingiza somo la Historia ya Tanzania na Maadili.
Baada ya kuona hatua hii, ambayo naona ni mwanzo mzuri, niliandika makala katika gazeti hili nikashauri kwamba somo la maadili lisimame lenyewe baadala ya kuchanganywa na historia ya Tanzania.
Tukumbuke kwamba somo la maadili ni somo mama, ni somo la msingi ambalo linajenga utu wa wanafunzi na utu wetu.
Mfanyabiashara maarufu Marekani, Warren Buffett, anasema: ‘’ Ukitaka kuajiri mtu uhakikishe ana sifa hizi tatu: kwanza, utaalamu katika fani husika, pili, uchapa kazi wa hali ya juu na tatu, uadilifu’’.
Anaendelea kusema, kama mfanyakazi huyo ana sifa mbili za kwanza bila hiyo ya tatu, atatumia hizo sifa mbili kuangamiza biashara yako.
Hivyo ni sahihi kusema kwamba somo la maadili ni somo mama kati ya masomo yote tunayofundisha shuleni.
Haitoshi kabisa kuwaachia wazazi na viongozi wa dini hili jukumu kubwa la kuwajenga watoto wetu katika uadilifu.
Vyuo vingi nje ya Tanzania vimetambua umuhimu wa somo hili, na hivyo kulifanya somo la lazima kwa wanafunzi wote wanaosoma katika vyuo hivyo.
Nimefundisha katika vyuo vitano huko Marekani ambavyo vyote vina somo la maadili kama somo la lazima kwa mwanafunzi yeyote anayetaka kuhitimu katika vyuo hivyo.
Baada ya kurudi kutoka huko miaka 13 iliyopita, nimeendelea kufundisha somo hili katika chuo kimoja kilichopo Chicago, Marekani kwa kutumia mtandao (online teaching and learning). Hata wakati huu naendelea kufundisha somo hilo katika chuo hicho.
Ninatamani sana kama wanafunzi wetu wa vyuo vikuu wangekuwa na somo hili ili liwatayarishe kwa masilahi ya familia zao na taifa kwa ujumla. Inaumiza akili na roho nikiona wenzetu walioendelea kiuchumi kiasi hicho wanatia mkazo somo la maadili katika shule zao zote.
Sisi hapa Tanzania tunaoendelea kukaangwa na umaskini ambao ungeweza kupunguzwa na watumishi wa umma walio waaminifu, hatulitilii maanani.
Ni kama sisi hatupo ‘serious’, yaani hatuoni uzito wa somo hili, hatupo ‘serious’ katika kujenga taifa lenye wafanyakazi waaminifu. Ikiwa ninakosea katika hili, naomba nisahihishwe kwa hoja mbadala.
Kama tukiwa na somo hili katika vyuo vyote, ni lazima basi liwepo katika vyuo vya kutayarisha walimu wetu.
Lengo liwe ni kutayarisha walimu ambao, kwanza, wote ni waadilifu katika utu na tabia zao, na pili, tutayarishe walimu ambao wamebobea katika somo hili ili waweze kulifundisha baada ya kuhitimu.
Tufanye yafuatayo. Tuanze na somo hilo kwa walimu wote. Somo hili litamjenga mwalimu mtarajiwa katika utu wake na katika tabia yake. Litamjenga kuelewa kwamba ualimu ni wito, na si kibarua cha kujipatia kipato.
Tatizo kubwa katika elimu yetu sasa ni kwamba tuna walimu wengi mno ambao wapo darasani kujipatia tu kipato.
Hawana wito wa ualimu. Katika mtindo huu ni muujiza kutegemea elimu bora itolewe shuleni.
Somo hili litamjenga mwalimu yeyote yule kuwa mtu mwadilifu. Ikumbukwe shule ni mwalimu na elimu ni mwalimu.
Mbobezi wa fizikia, hesabu na falsafa wa Kijerumani, Albert Einstein (1879-1955), anasema: mfano bora si tu ni njia nzuri ya kufundisha wengine, ni njia pekee ya kuwafundisha wengine.
Kwa maneno mengine, mwalimu anaweza kufundisha vizuri somo la maadili, lakini wanachojifunza wanafunzi ni jinsi yeye anavyoishi.
Maneno yote ya darasani hayatafua dafu ikiwa mwalimu wa somo lolote lile, haishi kiuadilifu.
Mwalimu anafundisha uadilifu au kinyume chake katika haya yafuatayo, na mengine ambayo wewe msomaji unaweza kuongeza.
Mambo hayo ni pamoja na vaa yake, anavyoingia darasani, anavyowajali wanafunzi, ana uso wa furaha, ukali, unyonge, au wa kirafiki, anawasaidiaje wanafunzi ambao wapo nyuma.
Ana uhusiano gani na wanafunzi wa jinsia tofauti na yake, anazingatia muda au hapana, anawajibikaje katika familia yake, na kadhalika. Haya yote na mengine ni kielelezo cha somo la maadili kwa wanafunzi wake.
Mwalimu akifanya vizuri katika mambo hayo, atakuwa mwalimu bora wa taifa letu.
Ni walimu wa mtindo huu waliotufundisha sisi miaka mingi iliyopita. Maisha yao yalikuwa darasa tosha kwetu katika uadilifu.
Nakumbuka wanafunzi wengi niliohitimu nao darasa la nane walichagua kuwa walimu kwa sababu walipenda yale waliyoyaona katika walimu wetu.
Tukitaka kuwa na taifa la watu waadilifu ni lazima tuwe na walimu waadilifu. Hakuna njia ya mkato.
Pili, kutokana na hawa walimu waadilifu wenye mifano mizuri ya maisha yao, tutawachagua wengine kati yao ili wajengwe kuwa wabobezi katika kufundisha somo hili.
Hawa wapewe somo la maadili chuoni kwa kiwango cha juu ili wawe wataalamu wa kufundisha somo hili.
Walimu hawa wabobezi watajifunza kwa mapana na undani zaidi somo la maadili ambalo ni tawi la elimu ya falsafa.
Watajifunza vizuri maadili ya tamaduni zetu na tamaduni na falsafa za makabila mengine na mataifa mengine.
Watakuwa wataalamu wa kutambua changamoto za uadilifu tunazozishuhudia katika maisha ya sasa.
Walimu hawa wabobezi ndio watakaopangwa kufundisha maadili kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Walimu wa aina hii wataweza kushirikiana na serikali, mashirika ya dini na wadau wengine katika kulea taifa lenye maadili.
Bila kuwa na somo hili katika ngazi zote za elimu, na bila kuwa na walimu waadilifu katika shule zetu, viongozi waadilifu katika mashirika ya dini na wadau wengine, itakuwa muujiza kutegemea kwamba taifa hili litakuwa na maendeleo chanya ya kiuchumi, kijamii, na kifamilia.
Hivi majuzi niikuwa na mazungumzo na wafanya kazi wa halmashauri kadhaa za nchi yetu, na wote wameniambia kwamba tuna tatizo kubwa la uadilifu katika utumishi wa umma.
Hali ni tete. Ukiingia katika siasa hali ni tete pia. Uadilifu umepungua sana. Ni wakati mwafaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoliojia na wadau wote tutoke usingizini ili kulinusuru taifa letu kutoka maangamizi yaletwayo na ukosefu wa uadilifu.