Walimu watambue hawako juu ya sheria

Hivi karibuni, kumeibuka wimbi la utoaji holela wa adhabu kwa wanafunzi shuleni.   Baadhi ya matukio yamesababisha madhara makubwa ikiwamo vifo na majeraha mabaya kinyume kabisa na sheria za nchi.

Matukio haya yanasikika kuanzia kusini mwa nchi hadi kaskazini, licha ya uwepo wa kanuni ya utoaji viboko GN namba 294 ya Julai 31, 2002 iliyozaa Waraka wa Elimu namba 24 wa 2002 kuhusu adhabu ya viboko.

Baadhi ya walimu wamekuwa wakiongozwa na jazba na mihemko katika kuwaadhibu watoto na matokeo yake huja kujuta,  pale wanaposababisha madhara makubwa katika mwili wa mtoto aliyemwadhibu au hata kusababisha kifo.

Sote tuliopita shule tunafahamu adhabu ya viboko huelekezwa kiganjani au kwenye makalio, sasa huu utaratibu wa mwalimu kuchapa kila mahali tena kuzidi idadi ya viboko vilivyoidhinishwa au kupiga vibao, mateke na ngumi unatoka wapi?

Walimu wetu ni lazima wafahamu kuwa pale adhabu ya viboko inapotolewa kinyume cha sheria, kanuni na taratibu, inageuka kuwa kosa la jinai chini ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code), kama ilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2022.

Ukisababisha kifo, unaweza kushitakiwa chini ya kifungu cha 195 na 197 cha kanuni ya adhabu, na kama utatiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia,  basi adhabu ya juu ni kifungo cha maisha na kama ni kukusudia basi adhabu ni kifo.

Lakini mwalimu akisababisha madhara makubwa mwilini kwa mtoto au mwanafunzi, anaweza kushitakiwa chini ya kifungu namba 225 cha kanuni ya adhabu ya 2022 na adhabu yake ni kifungo cha miaka saba jela.

Ninafahamu lengo la adhabu hizi ni kusaidia kuongeza utii shuleni hali inayofanya makosa ya utovu wa nidhamu kupungua na kuongezeka kwa nidhamu, lakini adhabu hii inapotolewa kinyume cha sheria, inageuka kuwa haramu.

Ingawa utoaji wa adhabu ya viboko ni jambo linalokubalika kisheria kupitia GN namba 294 ya 2002, lakini tafiti mbalimbali zinaonyesha adhabu hii huwajengea wanafunzi uoga na wakati mwingine kuongeza utoro na wanafunzi kuacha shule.

Mwanafunzi anapokuwa shule anapaswa kufuata sheria za shule ili kumwezesha kufuata masomo yake, lakini wapo ambao ni watovu wa nidhamu wanaosababisha walimu kuchukua hatua za kinidhamu ikiwamo adhabu ya viboko.

Sheria na waraka huo vinasema adhabu ya viboko inaweza kutolewa kwa utovu wa nidhamu uliokithiri au kwa makosa ya jinai yaliyotendeka ndani au nje ya shule na kuharibu sifa nzuri ya shule.

Sasa maelekezo ya sheria na waraka nilioutaja, zinataka adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja, lakini tunashuhudia watoto wanachapwa hadi viboko 10.

Lakini sheria na waraka huo vinataka adhabu itolewe na mwalimu mkuu au mwalimu mwingine atakayeteuliwa na mwalimu mkuu kwa maandishi. Tuwaulize walimu, hili linazingatiwa?

Utaratibu huo wa kisheria unataka mwanafunzi wa kike apewe adhabu ya viboko na mwalimu wa kike tu isipokuwa shule kama haina mwalimu wa kike, sasa tuwaulize walimu wetu, hili wanalitekeleza au ni uholela mtupu huko shuleni.

Waraka unataka kila mara adhabu ya viboko inapotolewa, adhabu iorodheshwe katika kitabu kilichotengwa kwa kusudi hilo na kuandika jina la mwanafunzi aliyepewa adhabu, kosa alilolitenda, idadi ya viboko na mwalimu aliyetoa adhabu.

Mwalimu mkuu anatakiwa atie saini katika kitabu kila adhabu hii inapotolewa na hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa anayekiuka kanuni hii,  na ni marufuku mwalimu yeyote kuonekana ameshika fimbo mikononi kwa lengo la kuadhibu.

Lakini sasa hivi ni kama nchi imekumbwa na pepo fulani au jinamizi, kiasi kwamba kanuni na taratibu hizi hazifuatwi wakati wa utoaji wa adhabu.

Baadhi ya walimu wetu hasa vijana, huamua kutoa adhabu nje ya ile iliyoidhinishwa ikiwamo kupiga kila mahali kwa ngumi na mateke na wakati mwingine kumchapa mwanafunzi maeneo hatarishi na kumsababishia umauti.

Tukio la hivi karibuni kabisa ni la mwanafunzi wa kike wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Mwasamba iliyopo Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Mhoja Maduhu (18) anayedaiwa kufariki Februari 26, 2025 kwa kipigo cha mwalimu.

Ni lazima walimu wetu watambue kuwa hawako juu ya sheria hivyo ni lazima waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake waheshimu kanuni.

Daniel Mjema anapatikana kwa namba:0656600900

Related Posts