Mijadala ya hivi karibuni imechochea mazungumzo ya dharura, huku wadau wakiishinikiza Serikali kuweka udhibiti mkali wa matumizi ya simu kwa watoto ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kingono na ukatili wa mtandaoni.
Teaser: Kitendo cha kumpa mtoto simu kinaonekana kama ishara ya uaminifu. Lakini katika kubadilishana huku, udhaifu mpya huibuka, ambapo ufikiaji wa mtandao bila uangalizi hufungua milango kwa hatari zisizoonekana zinazovizia nyuma ya kila upekuaji wa kioo.
Katika jamii za Tanzania, upepo mpya wa teknolojia unavuma kimyakimya.
Leo hii, utoto usio na hatia unakutana na hatari zilizojificha za kimtandao.
Mwanga hafifu wa vioo vya simu za mkononi umegeuka kuwa taswira ya kawaida, ukimulika nyuso changa zilizopotea kwenye udadisi. Hata hivyo, nyuma ya mchanganyiko huo ulio wazi, kuna hatari inayopuuzwa.
Mara nyingi, mabinti huvutiwa na simu za mama zao kwa ‘selfies’ za kucheza na kupekua chaneli za dijitali. Wanajikuta katika mstari wa mbele wa mabadiliko haya kimya kimya.
Wazazi, huongozwa na upendo na hamu ya kukuza ukaribu, bila kujua wanachanganya kati ya mapenzi na kuharibu mtazamo wa watoto dhidi ya vitendo haramu vilivyo katika teknolojia.
Kitendo cha kumpa mtoto simu kinaonekana kama ishara ya uaminifu. Lakini katika kubadilishana huku, udhaifu mpya huibuka, ambapo ufikiaji wa mtandao bila uangalizi hufungua milango kwa hatari zisizoonekana zinazovizia nyuma ya kila upekuaji wa kioo.
Mijadala ya hivi karibuni imechochea mazungumzo ya dharura, huku wadau wakiishinikiza Serikali kuweka udhibiti mkali wa matumizi ya simu kwa watoto ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kingono na ukatili wa mtandaoni.
Katika shule nyingi za sekondari, matumizi ya simu yamepigwa marufuku ili kudhibiti hali hiyo. Walimu na walezi wanapaswa kusimamia mawasiliano kati ya wanafunzi na wazazi wao.
Hata hivyo, mwenendo wa kutisha umejitokeza;– baadhi ya wazazi wanawapatia watoto wao simu kwa siri, hasa kwa mazungumzo ya usiku wa manane, bila kujua wanadhoofisha sheria zilizowekwa kwa usalama wao.
“Inasikitisha unapomkamata mwanafunzi na simu na akakueleza alipewa na mzazi wake,” anasema Marcus Baray, mwalimu mzoefu kutoka wilaya ya Karatu jijini Arusha.
Anaongeza: “Wazazi wanapaswa kuwa washirika katika vita hivi, si wawezeshaji. Nidhamu hufanikiwa zaidi pale familia na shule zinaposhirikiana.”
Katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Karatu, sera ya zamani ya kuharibu simu zinazokamatwa ilitumika kama onyo. Pamoja na kukusudiwa kubadilisha mwenendo wa wanafunzi, iliacha kutumika kwa hofu kwamba ilizalisha chuki badala ya kuwa katazo chanya.
Tatizo halisi linabaki yaliyomo kwenye vifaa hivyo mara nyingi hufichua taswira ya kutisha ya hatari zinazowakumba watoto.
“Hata katika madarasa ya juu, bado wanafunzi wana fikara za kitoto,” anasisitiza Baba Metian, mwalimu wa uchumi shuleni hapo.
Anaongeza: “Simu zimejaa maudhui ya wazi na ujumbe ambao mtoto hapaswi kuufikia. Ni bomu la muda linalosubiri kulipuka ikiwa hatutaingilia kati.”
Takwimu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, zinaonesha kuwa asilimia 67 ya watoto wa Kitanzania wenye umri wa miaka 12-17 wanamiliki simu bila usimamizi wowote.
Mbaya zaidi, asilimia mbili wanashawishiwa kushiriki shughuli za kingono mtandaoni kwa malipo, huku asilimia tatu wakipitia ukatili wa kingono kupitia mitandao ya kijamii.
Jennifer Calman, mwanasaikolojia kutoka shirika la C-Sema, anaeleza jinsi watoto wanavyogeuka wageni wa dijitali wanapojihisi wametengwa na familia zao.
“Watoto wanapotengwa na wazazi, wanatafuta afueni mahali pengine; mara nyingi kwenye mikono ya wahalifu wa mtandaoni. Hakuna mtoto anayepaswa kuvinjari mtandao bila mkono wa mwongozo,”anasema.
Mtaalam wa teknolojia, Yusuph Kileo anapendekeza matumizi ya teknolojia za udhibiti wa wazazi na kuanzishwa kwa Sera za Ulinzi wa Mtoto Mtandaoni ili kuimarisha ulinzi wa dijitali. “Simu za mkononi si chombo tu cha mawasiliano, ni lango. Wazazi wanapaswa kujua ni tovuti gani watoto wao wanatembelea, wanazungumza na nani, na muda gani wanakaa mtandaoni,”anaeleza.
Kuongezeka kwa umiliki wa simu za mkononi Afrika Mashariki kunafanya changamoto hii kuwa ngumu zaidi.
Katika muongo uliopita, matumizi ya simu yamepanda kutoka asilimia 30 hadi zaidi ya asilimia 70, hali inayoonekana pia Uganda. Ingawa simu zinaunganisha vijana na taarifa na huduma za afya, pia zinawaweka kwenye hatari za mtandao.
Utafiti wa Rakai Community Cohort Study nchini Uganda ulibaini kuwa wasichana wenye simu walikuwa na uwezekano mdogo wa kutumia kondomu, walijihusisha zaidi na tabia za kingono zisizo salama, na walikuwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya VVU.
Dunia ya mtandao inafuta mipaka kati ya unyanyasaji wa mtandaoni na wa moja kwa moja, ambapo wahalifu huwashawishi waathirika kutoka kwenye vyumba vya gumzo hadi kwenye mikutano ya ana kwa ana.
Unyanyasaji wa kingono wa watoto mtandaoni huacha makovu yanayodumu hadi utu uzima, yakiwasha uraibu, magonjwa ya akili na maisha ya utengano.
Mapambano dhidi ya unyanyasaji wa watoto mtandaoni yanahitaji mshikamano wa pamoja, ambapo kila mzazi, mwalimu na mtunga sera atakuwa mlinzi katika lango la dijitali.
Teknolojia peke yake haiwezi kulinda watoto. Kinga bora zaidi ni jicho la upendo la mzazi, sauti ya mwongozo ya mwalimu, na azimio thabiti la jamii inayokataa kuona watoto wake wanapotea katika vivuli vya mtandao.
Nchi zilizoendelea zimetekeleza mchanganyiko wa sheria, suluhisho za kiteknolojia na mikakati ya kijamii ili kuwalinda watoto dhidi ya madhara ya mtandao.
Kwa mfano, nchini Uingereza, Muswada wa Usalama Mtandaoni unalazimisha kampuni za teknolojia kutambua na kuondoa maudhui hatarishi, huku wakikabiliwa na adhabu kali kwa kutotii.
Itoshe kusema kwamba kulinda watoto katika zama za kidijitali kunahitaji mabadiliko ya kitamaduni, yanayothamini mazungumzo ya wazi, uaminifu wa pande zote, na uangalizi wa mara kwa mara.
Wazazi, walimu, na watunga sera wanapoungana katika dhamira hii, wanaunda ngao isiyoweza kuvunjika kwa watoto walio hatarini zaidi.