Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Stephen Wasira amesisitiza kuwa hakuna mtu yoyote ambaye anaweza kuzuia Uchaguzi Mkuu mwaka huu usifanyike na hao wanaotaka kuuzuia kama wametumwa wawaambia hao waliowatuma kwamba kazi hiyo ni ngumu na haitawezekana.
Akizungumza na wananchi wa Mbeya Mjini leo Machi 17,2025 katika mkutano wa hadhara, Wasira ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu uko pale pale na hakuna mtu yoyote anayaweza kuuzuia.
“Ni ngumu kuzuia uchaguzi mkuu kama ambavyo ni vigumu kufufua mtu aliyekufa.Katika historia aliyeweza kufufua waliokufa ni Yesu peke yake , wengine wanajaribu kwa kutumia jina lake lakini hakuna anayeweza.Hivyo waliotumwa kuzuia uchaguzi mkuu wamwambie aliyewatuma kazi ambayo wametumwa haitekelezeki kabisa.”
Wasira amesema haiwezekani kila siku kuwe na masharti mapya kutoka kwa hao ambao wanataka uchaguzi Mkuu usifanyike na kusisitiza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan baada ya kuingia madarakani amekuja na R nne ikiwemo R inayowakilisha maridhiano ambayo yamewezeasha hata waliokuwa wamekimbia nchi kurejea nchini na wako salama.
“Huko nyuma tumekuwa na matatizo na yanayotokea katika nchi mbalimbali,katika awamu ya tano wenzetu walikimbia nchi wakasema maisha yao yako hatarini wakakaa kule na Rais Samia alipochukua Madaraka akasema anataka maridhiano ya nchi.
“Nchi hii ni yetu wote uwe NCCR-Mageuzi,CCM, ACT-Wazalendo au CHADEMA.Hakuna nchi ambayo mnakubaliana kila kitu, hata Kanisani kuna wakati waumini hawakubaliani na Mchungaji au Padre wanapoona kuna mstari umekosewa.Rais akasema tufanye mabadiliko ya sheria mahali ambako tunaweza kufanya mabadiliko ili nchi iende kwa amani.Nchi katika kipindi cha miaka 60 hatujawahi kuahirisha uchaguzi na wala hatujawahi kupigana kwa namna yoyote ile. Hivyo Rais akaunda Kamati akakutana na vyama vyote akazungumza nao kuhusu maridhiano, vyama vyote vikakubali kasoro chama kimoja tu .
“Wakakubaliana mambo ya uchaguzi yafanyiwe marekebisho na Katiba mpya isubiri lakini kuna Chama kimoja ambacho kilitaka kisikilizwe peke yake. Hata hivyo Rais akaunda kamati maalumu ikiongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Abdulrhman Kinana na Chadema walikuja na hoja mbalimbali ambazo karibia zote zimefanyiwa kazi.
Pamoja na hayo yote Wasira amesema hakuna sababu za msingi za kuzuia uchaguzi hivyo ametoa rai kwa vyama vya siasa nchini kushiriki uchaguzi na wenye tabia ya kuweka mpira kwapani kwa kukimbia uchaguzi waache.“Kama wamemaliza kutukanana sasa watafute mgombea wao wa urais , sisi tayari tumemsimamisha Dk.Samia Suluhu Hassan.Waje kugombea wasiweke mpira kwapani maana kufanya hivyo ni kuogopa.”