WAZIRI SIMBACHAWENE,VIONGOZI TASAF WAENDELEA NA ZIARA YA KIMAFUNZO NCHINI AFRIKA KUSINI KUHUSU UTEKELEZAJI MIRADI

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora George Simbachawene ameongoza ujumbe wa viongozi waandamizi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo Shadrack Mziray katika ziara ya kimafunzo nchini Afrika ya Kusini.

Lengo la ziara hiyo ni kujifunza kuhusu namna bora ya utekelezaji wa mradi wa ajira za muda inayotekelezwa na TASAF na watakuwa nchini Afrika Kusini kwa siku tano kuanzia Machi 17 hadi Machi 23 mwaka huu.

Aidha ziara hiyo hiyo ya kimafunzo imefadhiliwa na Mfuko wa Nchi zinazotoa Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC FUND) ikijumuisha wadau mbalimbali wanaohusika moja kwa moja na utekelezaji wa mpango ikiwemo Ofisi ya Rais, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Fedha.

Mafunzo hayo yawawezesha Serikali pamoja na watendaji kupata weledi zaidi katika utekelezaji wa ajira za muda za TASAF katika awamu nyingine.

Awali kabla ya kuanza ziara hiyo, jana Machi 17 mwaka huu Waziri George Simbachawene na ujumbe wake walitembelea ofisi za ubalozi Tanzania nchini mjini Pretoria nchini humo kwa lengo la kusaini kitabu cha wageni pamoja na kusalimia watumishi.

Pia Waziri Simbachawene alifanya mazungumzona balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini Balozi James Bwana ambapo alimueleza kuwa balozi kuwa Ofisi yake imeboresha huduma kwa kujenga mifumo inayowezesha kutataua changamoto za kiutumishi kwa urahisi kwa watumishi wote wakiwemo walio katika balozi mbalimbali duniani.

Waziri Simbachawene alimweleza Balozi kuwa TASAF imewezesha kuwakwamua wananchi kiuchumi sambamba na kuboresha miundombinu katika maeneo mbalimbali ya vijijini ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, nyumba za walimu ili kurahisisha huduma za elimu kwa wanafunzi wa maeneo hayo.

“TASAF imekuwa suluhu ya kuwaondoa wananchi kwenye umasikini, hivyo,tunapokuja katika mafunzo kama haya inatusaidia katika kujiandaa na awamu nyingine za mradi wa kupambana umasikini,”alisema Waziri Simbachawene katika mazungumzo yake na balozi huyo.

Aidha kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini James Bwana alimshukuru Waziri kwa kazi nzuri inayofanywa na Wizara yake na kuahidi kutoa ushirikiano katika kipindi chote ambacho Waziri na ujumbe wake watakapokuwa nchini Afrika ya Kusini.

 

Related Posts