Deir al-Balah. Israel imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi ya anga eneo la Ukanda wa Gaza huku ikidai kuwa mashambulizi hayo yanalenga maeneo yenye makazi ya wapiganaji wa kundi la Hamas, na tayari yameua watu zaidi ya 100.
Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa mashambulizi hayo yameanza usiku wa kuamkia leo Jumanne Machi 18,2025, baada ya jitihada za kufikia mwafaka wa makubaliano ya awamu ya pili ya kusitisha mapigano kugonga mwamba.
Wizara ya Afya ya eneo la Gaza imethibitisha watu zaidi ya 100 kuuawa kwenye mashambulizi hayo huku mamia wakijeruhiwa.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema aliamuru mashambulizi hayo kwa sababu ya kukosekana kwa maendeleo katika mazungumzo yanayoendelea ya kurefusha usitishaji mapigano.

Maofisa wamesema operesheni hiyo haina kikomo na inatarajiwa kupanuka na kuendeleza mashambulizi zaidi eneo lote la Gaza.
“Kuanzia sasa, Israel itachukua hatua dhidi ya Hamas kwa nguvu kubwa zaidi za kijeshi,” ilisema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Netanyahu.
Shambulio hilo la ghafla la usiku lilivunja kipindi cha utulivu wa muda mfupi na kuongeza uwezekano wa kurejea mapigano katika vita vya miezi 17, ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 48,000 na kusababisha uharibu wa majengo na vitu mbalimbali kote Gaza.
Pia, shambulio hilo lilizua maswali kuhusu hatima ya mateka wapatao 24 wa Israeli wanaoendelea kushikiliwa na Hamas, ambao bado wanaaminika wapo hai.
Katika taarifa, Hamas imelaani na kulielezea shambulio hilo kama “uchokozi wa Israeli usio na sababu”, na kusema kuwa hatua hiyo imehatarisha usalama wa mateka wa Israeli waliopo Gaza.
Hakukuwa na majibu ya haraka kutoka Marekani. Hata hivyo, mwishoni mwa wiki, mjumbe wa Marekani Steve Witkoff, ambaye amekuwa akiongoza juhudi za upatanishi kwa kushirikiana na Misri, Qatar, alionya kuwa Hamas lazima iwaachilie mateka la sivyo italipa gharama kubwa.
Ofisa mmoja wa Israel, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa operesheni ilikuwa bado inaendelea, alisema Israeli ilikuwa inashambulia vikosi vya kijeshi vya Hamas, viongozi wake na miundombinu yao na ilikuwa inapanga kupanua operesheni hiyo zaidi ya mashambulizi ya anga.
Ofisa huyo aliituhumu Hamas kwa kujaribu kujijenga upya na kupanga mashambulizi mapya dhidi ya Israeli, madai ambao Hamas haijathibitisha ama kukataa.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amejiapiza huku akisema milango ya kuzimu itafunguka Gaza ikiwa mateka ambao ni raia wa Israeli hawataachiliwa.

“Hatutakoma kupigana hadi mateka wetu wote warudi nyumbani na tufanikishe malengo yote ya vita,” amesema Katz.
Milipuko ilisikika eneo lote la Gaza, na Wizara ya Afya ya Gaza ilisema angalau watu zaidi ya 100 wameuawa katika wimbi jipya la mashambulizi ya anga.
Shirika la Ulinzi wa raia la eneo hilo limesema vikosi vyake vinapata ugumu katika shughuli za uokoaji kwa sababu yalilengwa maeneo mengi kwa wakati mmoja.
Mazungumzo ya awamu ya pili
Mashambulizi hayo yamekuja miezi miwili baada ya kufikiwa kwa usitishaji mapigano kwa muda.
Katika kipindi cha wiki sita, Hamas iliwaachilia mateka takriban 36 kwa kubadilishana, huku wafungwa 2,000 wa Kipalestina nao wakinufaika kwa kuachiliwa awamu ya kwanza ya makubaliano ya usitishaji mapigano hayo.
Hata hivyo, tangu usitishaji huo wa mapigano ulipoisha wiki mbili zilizopita, pande hizo mbili zimeshindwa kukubaliana juu ya njia ya kuendelea na awamu ya pili inayolenga kuwaachilia mateka wapatao 60 waliobaki na kumaliza vita kabisa.
Netanyahu ameendelea kutishia kurejelea vita, na mapema mwezi huu alisitisha kuingia kwa chakula na misaada yote katika eneo la Gaza lililozingirwa ili kuilazimisha Hamas kuachia mateka wake.
“Hii inafuatia Hamas kukataa mara kwa mara kuwaachilia mateka wetu na kukataa ofa zote ilizopokea kutoka kwa mjumbe wa rais wa Marekani, Steve Witkoff, na wapatanishi wengine,” ofisi ya Netanyahu imesema.
Taher Nunu ambaye ni Ofisa wa Hamas, alikosoa mashambulizi ya Israeli akisema kuwa: “Jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na mtihani wa kimaadili: aidha inaruhusu kurejea kwa uhalifu unaofanywa na jeshi la uvamizi au inasimamia ahadi ya kumaliza uvamizi na vita dhidi ya watu wasio na hatia Gaza.”
Tangu kuanza kwa vita hivyo, Oktoba 7, 2023, Hamas ilipoivamia Israel na kuua takriban watu 1,200 huku ikiwachukua mateka wengine 250. Israeli ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya kijeshi ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 48,000, kwa mujibu wa maofisa wa afya wa eneo hilo, na kulazimisha takriban asilimia 90 ya wakazi wa Gaza kuyahama makazi yao.
Wizara ya Afya ya Gaza haitofautishi kati ya raia na wapiganaji, lakini inasema zaidi ya nusu ya waliouawa ni wanawake na watoto.
Usitishaji mapigano ulikuwa umeleta nafuu kidogo Gaza na kuruhusu mamia ya maelfu ya Wapalestina waliopoteza makazi kurejea kwenye mabaki ya nyumba zao.
Hata hivyo, eneo hilo linakabiliwa na uharibifu mkubwa, bila mipango ya haraka ya kujenga upya. Kurejea kwa vita kunatishia kubatilisha maendeleo yoyote yaliyofikiwa katika wiki za hivi karibuni kuelekea kupunguza mgogoro wa kibinadamu wa Gaza.
Kurejea kwa mapigano kunaweza pia kuzidisha mgawanyiko mkubwa wa ndani ya Israeli juu ya hatima ya mateka waliobaki. Mateka wengi walioachiliwa na Hamas walirejea wakiwa wamedhoofika na walielezea hali ngumu walizopitia walipotekwa.
Wamekuwa wakiwasihi mara kwa mara viongozi wa Serikali kuendelea na usitishaji mapigano ili kurejesha mateka wote waliobaki, huku makumi ya maelfu ya raia wa Israeli wakishiriki maandamano makubwa katika wiki za hivi karibuni wakidai usitishaji mapigano na urejeshaji wa mateka wote.
Tangu usitishaji mapigano Gaza ulipoanza katikati ya Januari, vikosi vya Israeli vimewaua makumi ya Wapalestina, ambao jeshi linasema walikaribia wanajeshi wake ama kuingia maeneo yasiyoruhusiwa.
Misri, Qatar na Marekani zimekuwa zikijaribu kupatanisha hatua zinazofuata katika usitishaji mapigano. Israeli inataka Hamas kuwaachilia nusu ya mateka waliobaki kwa ahadi ya kufanya mazungumzo ya kufanikisha usitishaji mapigano wa kudumu.
Hamas, kwa upande wake inataka kufuata makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa awali, ambayo yanataka mazungumzo kuanza kuhusu awamu ya pili ya makubaliano hayo, ambapo mateka waliobaki wataachiliwa na vikosi vya Israeli vitaondoka Gaza. Hamas inaaminika kushikilia mateka 24 walioko hai na miili ya wengine 35.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.