Dar es Salaam. Uchunguzi umebaini kuwapo kwa wafanyabiashara wengi wa kigeni wanaofanya biashara zinazofanywa na wazawa huku wakiuza bidhaa kwa bei ya chini jambo ambalo linaondoa ushindani sokoni.
Hayo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kamati ya kufuatilia na kuhakikisha raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa maeneo ya Kariakoo, iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Edda Lwoga.
Taarifa hiyo iliyowasilishwa jana jijini Dar es Salaam pia imebaini wageni kutumia vitambulisho vya uraia vya Watanzania kusajili biashara zao, pia ilibaini katika maduka 75 wamekutwa raia wa kigeni 152 waliajiriwa, huku asilimia 97 kati yao wakijihusisha na biashara za rejareja, 28 wakiishi nchini kinyume na sheria na 24 wakiondolewa nchini.
Kamati hiyo iliundwa Februari 5, 2025 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeagiza, ufanyike uchunguzi ili kuhakikisha raia wa kigeni hawajishughulishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wenyeji.
Kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe 15 ilifanya kazi kwa siku 30, ambapo pamoja na mambo mengine ina jukumu la kufuatilia utoaji leseni za biashara kwa wazawa na wageni sambamba na kusajili wafanyabiashara ili kuwa na kanzi data yao.
“Katika wageni hao 31 tuliowabaini hatua stahiki zilichukuliwa na idara ya uhamiaji na 24 waliondolewa nchini wakati kamati ikiendelea na kazi yake,” amesema Profesa Lwoga.
Pia kamati hiyo ilibaini kuwapo kwa wimbi la wageni wanaoingia nchini kwa kigezo cha kuwa wataalamu na badala yake wanaishia kufanya kazi zinazotakiwa kufanywa na wazawa.
“Kamati ilibaini pia wageni wanauza bidhaa kwa bei ya chini hivyo kuwafanya wazawa kushindwa kuhimili ushindani wa soko na ilibaini udhaifu katika upangishaji wa wafanyabiashara,” amesema Profesa Lwoga.
Hiyo ni baada ya wageni kuwaondoa wazawa katika maeneo waliyopanga kwa kulipa kodi kubwa zaidi kupitia malipo yajulikanayo kama kilemba.
Kupitia hilo kamati ilipendekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuanzisha kanda maalumu ya biashara Kariakoo na kanzi data, ili kulifanya eneo hilo kuwa na hadhi maalumu ya biashara.
“Hilo liende sambamba na kutenga maeneo ya biashara za jumla na rejareja, kuwa na eneo moja la utoaji huduma za Serikali, pia inashauriwa wizara ya viwanda na biashara ipitie na kurekebisha sera ya maendeleo ya biashara ya mwaka 2003 toleo la mwaka 2023 ili ianishe aina ya biashara ambazo wageni wanapaswa kufanya,” amesema.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo aliitaka idara ya ajira na uhamiaji kufanya operesheni kubainisha watu wanaofanya biashara kinyume na taratibu.
“Tume ya ushindani na TBS hakikisheni mnafanya operesheni ya pamoja kufuatilia ya malalamiko ya uwepo wa bidhaa ambazo hazina ubora na zinaharibu biashara. Kila baada ya miezi sita tukutane wadau tujadili hili,” amesema.
Akizungumzia ripoti ya kamati, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi amesema matumaini yake ni kuona Serikali inazingatia yale yaliyotokana na ripoti ya tume iliyokuwa imeundwa, ili Kariakoo iwe sehemu nzuri ya biashara.
Mfanyabiashara Selemani Kifaranga amesema huenda kuna watu wamekuwa wakiwaleta Wachina hao, kwani ni ngumu wao kuja moja kwa moja na kuanza kazi.
“Kwa sababu Serikali wenyewe wameliona sisi tumefurahi,” amesema Kifaranga.
Malalamiko ya raia wa kigeni kufanya shughuli za wazawa yamekuwa yakitolewa kwa vipindi tofauti na wafanyabiashara wa soko hilo.
Aprili mwaka jana katika Baraza la Biashara la jiji la Dar es Salaam, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Omary Yenga alisema soko ni kitu muhimu katika ukuaji wa uchumi na kama Watanzania ni vyema kulilinda.
Alisema kuruhusu kuingiliwa kwa soko hilo na watu wa nje wenye teknolojia zilizoendelea na kuwaacha wafanye kazi ndogo za watu wa ndani ni kuua uchumi na si kuukuza.
“Serikali iangalie hili suala la Wachina kufanya biashara ndogondogo, wawekezaji waje kwa ajili ya uwekezaji waje na uwezo na si kuingilia kazi za zinazoweza kufanywa na Watanzania,” alisema Yenga.
Mfanyabiashara, Riziki Ngaga alisema kwa sasa kumekuwa na wimbi la watu wanaokuja kutoka mataifa mbalimbali, wanaoleta bidhaa katika makontena huku wakichagua namna ya kuziuza.
Alisema baadhi wamekuwa wakiuza kwa namna ambayo inaweza kuifanya Serikali kupata mapato au kukosa mapato.
“Wachunguzwe haiwezekani Mchina anakuja kufanya biashara ndogo, kiuchumi nchi inakua na inatarajiwa kurithi teknolojia, mgeni anapokuja kufanya biashara ndogo, Serikali haitengenezi ajira,” alisema Ngaga.
Alisema ni vyema kuwapo kwa mpango wa kutengeneza wafanyabiashara wakubwa ili nchi iweze kufanya biashara kimataifa kwa kuangalia sera na sheria zilizopitwa na wakati, kwani ndiyo zinafanya wageni badala ya kuwa wawekezaji wanakuwa wachuuzi.
“Tunatarajia wawekeze katika viwanda kufanya miradi mikubwa ya barabara, tunapata wawekezaji ambao wanakuja kufanya biashara za kutandaza bidhaa kama wamachinga,” alisema Ngaga.
Akijibu hoja hiyo wakati akihitimisha baraza, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema Tanzania inapopokea wageni kuja kuwekeza huwa kuna sheria zinazomsimamia, pia zipo taratibu zinazomruhusu mfanyabiashara wa ndani kutumia fursa ya mwekezaji ili aweze kufanya biashara zake.
“Malalamiko ni watu wa nje kujihusisha na biashara za kichuuzi ambazo zingeweza kufanywa na wafanyabiashara wa ndani, tumeyapokea na eneo lililotajwa ni Kariakoo,” alisema Chalamila na kuongeza
“Tutakwenda kuanza msako wa kawaida na kutoa elimu kubwa ili wafanyabiashara wa ndani waweze kujua namna gani wanaweza kunufaika na nchi yao, na wanaotoka nje kuja kuwekeza waweze kusaidia wafanyabiashara wa ndani kupata mali zinazozalishwa na uwekezaji wao,” alisema Chalamila.