Dereva Mtanzania akamatwa Sudan Kusini, wataka Sh938 milioni wamwachie

Dar es Salaam. Zimepita siku 31 tangu dereva Mtanzania, Juma Maganga (45) ashikiliwe na linalodaiwa kuwa Jeshi la Polisi Mji wa Juba nchini Sudan Kusini, akidaiwa kugonga mtu (mwanaume) ambaye alifariki dunia.

Kufuatia hilo, polisi na familia ya marehemu imedai fidia ya zaidi ya Pauni ya Sudan kusini 213.09 (zaidi ya Sh925.075 milioni) kutoka kwa familia ya dereva. Kutokana na hilo mmiliki  wa gari aliyepo Tanzania wakiomba Serikali iingilie kati suala hilo.

Maganga anadaiwa kumgonga mwanaume huyo katika eneo la Juba, Sudan Kusini, Februari 14, 2025 wakati wakipeleka mahindi ya msaada nchini humo.

Jambo hilo limefanya gari na mzigo uliokuwamo kushikiliwa hadi leo Jumanne, Machi 18, 2025 huku matumaini yakiendelea kufifia kutokana na fedha zinazohitajika kama fidia kuongezeka kila siku.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, mmiliki wa gari hilo, Gabriel Kiliki amesema baada ya tukio, waliambiwa baba wa marehemu anataka fidia Dola 3,200 (Sh8.47 milioni) ili Maganga aachiwe.

Pia, imedaiwa baba huyo alidai marehemu alikuwa na wake watatu ambapo kila mmoja wao ataeleza mahitaji yao ya fidia ambayo yatawasilishwa kwa mmiliki na familia ya dereva ili yalipwe na ikiwa yatatimizwa wataachia gari pamoja na Maganga ataruhusiwa kuondoka nchini humo.

“Lakini kabla hili halijatimizwa Machi 16, 2025 nilitumiwa karatasi nyingine ya fedha ninazotakiwa kulipwa zikiwa zimeongezeka hadi pauni ya Sudan milioni 213.06 (zaidi ya Sh938.71 milioni).

Kwa mujibu wa karatasi hizo ambazo pia Mwananchi ilizipata zilikuwa zimeunganishwa na gharama zilizotumika katika kuongoza msiba wa marehemu huyo na fidia.

Katika upande wa mchanganuo wa fidia walitaka pauni za Sudan 161.5 milioni ilipwe kwa familia, msiba siku ya pili ulitumia Sh10.09 milioni, siku nyingine ya msiba ilitumia pauni 19.24 milioni na gharama nyingine zikiwa Pauni za Sudan milioni 21.46.

“Kiukweli tunafuatilia bado lakini tunaona kumtoa kwa dhamana imekuwa kazi, sasa tunatafuta mwanasheria ili aweze kwenda huko ili turuhusu wampeleke mahakamani ili kesi isomwe na kuamriwa huko,” amesema Kiliki.

Amesema kama mmiliki mara zote amekuwa akiwasiliana na mtoto wa Maganga ambaye alikuwa kama kondakta kwenye gari wakati wakisafirisha mahindi ya msaada kwenda nchini Sudan Kusini katika eneo la Juba.

“Mpaka sasa mzigo bado upo kwenye gari wamezuia hata gari isishushe, tulienda nao hadi WFP (Shirika la Chakula Duniani) ili tushushe warudi na gari wakakataa na sasa wanasema kama hatutalipa hiyo fedha gari langu litatolewa kwa familia ya mtu aliyegongwa,” amesema.

Kiliki amesema walishatuma zaidi ya Sh1 milioni kwa askari waliomshikilia ili wamuachie, lakini mpaka sasa bado kashikiliwa.

“Kila tunapowasiliana na hao askari Polisi wa huko wanakuwa wanataka hela lakini hawakamilishi tunachokubaliana, hata hivyo tunaendelea kuwasiliana na Mwenyekiti wa Madereva wa Malori wa Afrika Mashariki anaitwa Sudi, anasaidia kuwasiliana na Polisi wa hapo,” amesema.

Mbali na mtoto wa dereva Maganga ambaye huwasiliana na watu waliopo Tanzania muda mwingi pia kuna madereva wengine wanne ambao nao wapo huko wanashughulikia.

Kutokana na tukio hilo,  Mwananchi ilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mindi Kasiga ili kujua kile kinachoendelea ambapo ameomba atafutwe Sheiba Bulu ambaye Ofisa habari wizara hiyo.

Kwa upande wake, Sheiba amemtaka mmiliki wa gari kupeleka malalamiko hayo ofisini kwao ili wayatafutie majibu: “Mwambie alete malalamiko tuyaone, tukutafutie majibu wewe mwandishi,”

Mwananchi limemrejea tena baada ya majibu hayo ya Serikali, mmiliki wa gari Kiliki amesema tayari malalamiko hayo yaliwasilishwa katika ofisi za wizara hiyo Dodoma huku akiahidiwa usaidizi.

Mke wa dereva huyo, Rehema Mongi amesema baada ya tukio hilo, mume wake pamoja na mwanaye walipigwa na wananchi jambo ambalo lilifanya wapelekwe kituo cha afya kabla ya kupelekwa gerezani.

“Walimuachia mwanangu ili apate nafasi ya kutoa taarifa kwetu, wamekuwa wakitaka hela huko, tunatuma lakini hawamtoi. Hela inapotumwa mwanangu akienda Kituo cha Polisi waliposhikiliwa awali, wanaambiwa askari aliyepokea fedha hayupo, mara hayupo zamu mara kaenda likizo,” amesema.

Amesema jambo hilo lina utata kwani wao wanasema ajali ilimuhusisha mwanaume lakini kwenye taarifa ya Polisi inadaiwa wameandika aliyekufa ni mwanamke.

“Tunaomba msaada Serikali itusaidie kumuokoa Mtanzania mwenzetu, nimeambiwa ana kidonda kikubwa, anaumwa sana lakini bado wamemuweka ndani kama familia tunapitia wakati mgumu sana, kwani kama hela tumeshachanga zaidi ya mara moja na inayoombwa sasa ni kubwa sana hatuwezi kuimudu.”

“Mpaka sasa hatuelewi hatima yake itakuwaje maana hatuna taarifa yoyote zaidi ya kutakiwa kulipa hiyo Sh210 milioni ya Sudan na sisi hatuna uwezo wa kuilipa,” amesema.

Maganga ni baba wa watoto sita ambapo wawili kati yao wanajitegemea huku wanne wakiwa bado wanahitaji huduma yake na mpaka sasa hawajui itakuwaje.

Alipotafutwa mwenyekiti wa madereva wa malori, Hassan Dede amesema taarifa hizo nao wamekuwa wakizisikia lakini wanashindwa kuzishughulikia kwa sababu Maganga si mwanachama wao.

Hiyo inaweka ugumu kwao kujua sehemu ya kuanzia kwani wanashindwa kupata taarifa za kina juu ya kile kilichotokea.

“Ndiyo maana kila siku tunawahimiza wajiunge katika chama ili ikitokea tatizo kama hili kunakuwa na wepesi wa kusaidia, wale waliokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo walipatiwa msaada wa haraka kwa sababu ni wanachama, hivyo hatuna taarifa zake wala za mwajiri wake hatumjui sasa tunaanzia wapi, angekuwa mwanachama haya yote tungeyajua,” amesema Dede.

Related Posts