RCC Kigoma yaridhia kugawanywa majimbo manne ya uchaguzi

Kigoma. Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kigoma (RCC) imeridhia kugawanya majimbo manne ya uchaguzi mkoani Kigoma ambayo ni Kigoma Mjini, Kasulu Vijijini, Uvinza na Kibondo.

Maazimio hayo yalipitishwa na kikao maalumu kilichoketi Machi 17, 2025, ambapo yaliyowasilishwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zikitaka.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Kakonko (DCC) iliazimia na kupendekeza kubadilishwa jina la jimbo la Buyungu na kuitwa Kakonko.

Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Kigoma, Hussein Moshi amesema katika jimbo la Muhambwe Kamati ya ushauri DCC Kibondo ilipendekeza Wilaya ya Kibondo kuligawa jimbo hilo kuwa majimbo mawili la Kibondo Mashariki na Kibondo Magharibi.

Amesema katika Halmashauri ya Uvinza, mapendekezo yaliyowasilishwa ni jimbo la Kigoma Kusini ligawanywe na kupata jimbo la Uvinza pamoja na Buhingu.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye akiongoza kikao cha RCC kuhusu pendekezo wa ugawaji majimbo mkoani Kigoma.

Mapendekezo ya jimbo la Kigoma mjini yaliyowasilishwa na DCC ilikuwa kuligawa ili kupata jimbo la Kigoma na jimbo jipya la Ujiji.

Aidha, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Kamati ya Ushauri ya Wilaya ilipendekeza jimbo la Kasulu Vijijini ligawanywe ili kupata jimbo la Makere na Buyonga.

Kutokana na mapendekezo hayo wajumbe wa RCC wameridhia na yatakayowasilishwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya maamuzi.

“Kamati imepitia na imeridhia na kupitisha mapendekezo yote yaliyowasilishwa na halmashauri na kinachosubiliwa ni Tume kupitia mapendekezo na kufanya uamuzi kupitia vigezo vilivyowekwa katika mchakato huu. Kama tume itaridhia… mapendekezo yaliyopitishwa yatakubalika kutakuwa na ongezeko la majimbo,” amesema Moshi.

Andengenye amesema mchakato huo umezingatia vigezo vyote pamoja na vipaumbele kuendana na mahitaji ya kila halmashauri ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Mkazi wa Kigoma Ujiji, Haruni Cuabandi amesema ugawaji huo utarahisisha utendaji kwa wabunge wa majimbo hayo, kwani hivi sasa wanawakilisha watu wengi na eneo kubwa zaidi hali inayochelewesha maendeleo.

Related Posts