Unguja. Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), limeanza mchakato wa ulipaji wa fidia kwa wananchi waliotoa vipando (mazao) yao kwa ajili ya kupisha mradi wa nyumba za makazi Chumbuni Unguja.
Akizungumza katika kikao cha uhakiki na maelekezo kwa wahusika Machi 18, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Sultan Said Suleiman amewahakikishia wananchi hao kuwa hakuna atakayedhulumiwa na malipo hayo yataanza kulipwa hivi karibuni, baada ya kumaliza uhakiki.
“Kwa wale ambao hawajakamilisha taratibu za kulipwa ikiwemo kufungua akaunti, mnapaswa kufanya hivyo ili kuingiziwa fedha zenu,” amesema Sultan bila kutaja kiwango cha fidia kitakachotolewa wala jumla ya watakaolipwa fidia hiyo.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Amina Malik Protas amelishukuru shirika hilo kwa kutimiza ahadi yake iliyoitoa hapo awali ya kulipwa fidia za vipando vyao.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuelekeza maendeleo Chumbuni pamoja na kutekeleza ahadi ya kutulipa vipando vyetu jambo hili linaonyesha uungwana na kutujali wananchi,” amesema Amina.
Naye Mkuu wa Kituo cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) eneo hilo, Suleiman Ali Mzee ametoa wito kwa wananchi hao kutoendelea tena na shughuli za kilimo katika baada ya kulipwa fidia zao, ili kuepusha migongano baina yao.
Katika hatua nyingine Sultan, akiwakabidhi eneo washauri elekezi walioshinda zabuni ya mradi huo kampuni ya Mecon Arch Consult Ltd pamoja na Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) amewataka kuhakikisha wanausimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kulinda upotevu wa fedha za Serikali.
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Mecon, Moses Mkony amesema atahakikisha wanasimamia mradi huo kama walivyokubaliana kwenye mkataba.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi Chumbuni utasimamiwa na kampuni ya Wehian Hutan Ltd kutoka China na unatarajiwa kuchukua miezi 14 hadi kukamilika.