Vita DRC ‘imezalisha’ wakimbizi 100,000 – Global Publishers




Umoja wa Mataifa (UN) unaripoti kuwa mapigano ya silaha katika jimbo la Ituri, Kaskazini-Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yamesababisha watu takriban 100,000 kufurushwa kutoka makazi yao na kuwa wakimbizi.

Mapigano kati ya kundi la waasi wa M23 na Jeshi la Serikali ya DRC (FARDC) pia ni chanzo kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi katika jimbo la Kivu Kusini.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), ghasia katika maeneo ya Djugu, Irumu, na Mambasa zimesababisha vifo zaidi ya raia 200 kati ya Januari na Februari 2025.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, mpango wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO, umesema waasi wa M23 wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya kijeshi mashariki mwa DRC kwa msaada wa jeshi la Rwanda na wamechukua udhibiti wa sehemu kubwa za majimbo ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu.

OCHA imeonya kuwa vurugu inasababisha nchi hiyo ya Maziwa Makuu kushuhudia moja ya migogoro migumu zaidi ya kibinadamu duniani, huku zaidi ya watu milioni 21 wakiwa na mahitaji mengi.


Related Posts