Mpanzu, Kibu wampa mzuka Fadlu

KOCHA wa Simba, Fadlu Davids ameeleza mkakati wake wa kiufundi katika safu ya ushambuliaji akisisitiza umuhimu wa kubadilishana nafasi kwa wachezaji wa mbele ikiwemo Elie Mpanzu, Kibu Denis na Charles Jean Ahoua ili kuzalisha mashambulizi ya aina tofauti. 

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini ambaye anachanga karata zake kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, amesema mfumo wa kushambulia si wa mchezaji mmoja kudumu eneo moja  hutegemea na mbinu ya mpinzani.

“Tunajaribu kuwaweka wachezaji wetu katika nafasi tofauti kulingana na mpinzani tunayekutana naye. Wakati mwingine upande wa kushoto, wakati mwingine kulia inategemea na mpango wa mchezo ulivyo,” alisema Fadlu. 

Kocha huyo alifafanua kuwa mabadiliko ya nafasi yamekuwa yakiwasaidia katika michezo mingi ikiwemo uliopita wa kiporo dhidi ya Dodoma Jiji ambao waliibuka na ushindi wa mabao 6-0 akimtaja Kibu Denis kuwa mfano wa mchezaji aliyebadilika kutoka upande mmoja kwenda mwingine ili kuepuka ulinzi mkali wa wapinzani.

“Kibu Denis alifungiwa njia wakati fulani na tuliamua kuwabadilisha nafasi. Hii ni sehemu ya mfumo wetu wa mzunguko na kubadilika kitu ambacho ni muhimu kwa wachezaji wetu wanne wa mbele,” aliongeza. 

Safu ya ushambuliaji ya Simba imekuwa na matokeo mazuri ikiongozwa na kiungo mshambuliaji, Charles Ahoua ambaye tayari ameifungia timu mabao 12 huku akiwa na asisti sita na kuwa kinara wa mabao kwenye ligi.

Leonel Ateba amefunga mabao manane, huku Steven Mukwala akiwa nayo tisa – wote hao ni washambuliaji wa kati. Kwa upande mwingine Kibu amefunga mabao mawili na asisti mbili, wakati Mpanzu aliyeingia wakati wa dirisha dogo akiwa na mabao matatu na asisti tatu. Mbali na safu ya ushambuliaji, Fadlu pia aliwasifu mabeki wake wa pembeni kwa kusaidia mashambulizi na kuhakikisha timu inakuwa na uwiano mzuri wa kushambulia na kujilinda.

“Na bila shaka, mabeki wetu wa pembeni wamekuwa wakifanya kazi nzuri pia,”  alisema. 

Mabadiliko ya mbinu Simba yanaonyesha jinsi Fadlu anavyopania kuifanya safu ya ushambuliaji kuwa hai, isiyotabirika na yenye uwezo wa kuvunja ukuta wa timu pinzani kwa urahisi.

Katika ligi Simba ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 57 ni timu ya pili pia kwa kuwa na mabao mengi zaidi kwenye ligi (52), nyuma ya Yanga ambayo inaongoza ikiwa na mabao sita zaidi huku ikiwa na pointi 58. Kwa upande wa kimataifa, Simba imefunga mabao manane katika michezo ya hatua ya makundi msimu huu.

Related Posts