SINGIDA Black Stars inachekelea usajili wa kumshusha nchini mshambuliaji Jonathan Sowah, lakini wakubwa wamemuona ikiwemo Yanga na hesabu mpya ni kwamba imemuachia msala kocha wa timu hiyo, Miloud Hamdi kufanya uamuzi ili mabosi wa klabu wamalize kazi.
Yanga imeshawishika na nguvu ya Sowah akiwa ameingia Tanzania kupitia usajili wa dirisha dogo ambapo amecheza mechi saba akifunga mabao saba.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mabosi wamemuachia Hamdi kufanya uamuzi kwa kuwa anamjua Sowah kuanzia alipofika nchini walipokutana Singida Black Stars.
Ingawa Hamdi hakufanya kazi na Sowah kwa kumuona akicheza mechi, lakini kocha huyo atatumia mechi zilizobaki za Ligi Kuu kufanya uamuzi wa mwisho juu ya mshambuliaji huyo raia wa Ghana.
Yanga iliwahi kumhitaji Sowah walipokutana naye akiwa na Medeama ya Ghana, timu hizo zilipokutana katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Hata baada ya Sowah kutimkia Uarabuni, Yanga bado iliendelea kuiwinda saini yake, kabla ya Singida kuwawahi na kumsajili Desemba mwaka jana.
“Kweli Sowah, namba zake zinatufikirisha sana, kwa haki kabisa ukiangalia kuanzia dirisha dogo ni mchezaji gani amefanya makubwa jibu ni moja tu Sowah,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga na kuongeza;
“Tumemuachia kocha atuambie anamuonaje. Alifanya naye kazi kule Singida ingawa kwa muda mfupi lakini kama akisema tumsajili tutazungumza na Singida na mambo yatakuwa sawa.”
Bosi huyo aliongeza kwamba pia mbali na maamuzi hayo ya Sowah Yanga pia imemuachia nafasi kocha wao kutafuta nafasi ya mshambuliaji huyo kwwenye kikosi chake kwa kufanya maamuzi ya mchezaji gani aachwe wa kigeni.
“Unajua nafasi za wachezaji wa kigeni zinatubana, lakini pia kocha ataangalia akisema hapohapo kwamba tumsajili Sowah pia afanye uamuzi ni mchezaji gani tumuache kwenye kikosi cha sasa.
Yanga ilikuwa inapiga hesabu za kumuacha mshambuliaji Kennedy Musonda aliyefunga mabao matatu katika ligi aidha kumtoa kwa mkopo au kuachana naye moja kwa moja mwisho wa msimu huu.