Yanga kumekucha CAS, Bodi ya Ligi yakomaa

SAKATA la kuahirishwa mechi ya Kariakoo Dabi, Yanga dhidi ya Simba limechukua sura mpya na tafsiri nyepesi ni kama mambo ya yamekucha rasmi kwani awali ilionekana kama masihara.

Dabi hiyo katika Ligi Kuu Bara duru la pili, imeendelea kupigwa nje ya uwanja na sasa kuna mbio zinapigwa kwa hesabu za kisheria baada ya vinara wa ligi, Yanga kufanya kweli rasmi kufungua kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) jijini Lausanne,Uswisi.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Yanga imewasilisha rasmi kesi hiyo CAS, jana Jumatatu mchana baada ya kutoridhishwa na majibu ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya barua yao. Lakini hakuna kiongozi yoyote aliyekubali kunukuliwa kwa kutajwa jina juu ya sakata hilo kwa madai kuwa wanahofia mamlaka za nchi na zile za soka la Tanzania.

Huku wakisisitiza CAS itawapa TFF na Bodi taarifa ya kupokea malalamiko hayo.

CA 04

Hatua hii imekuja kufuatia mchezo wa Yanga na Simba uliokuwa upigwe Machi 8,2024 kuahirishwa, ambapo siku moja kabla ya mchezo huo utata ulianza baada ya Simba kudai kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na watu wanaodhaniwa kuwa ni makomandoo wa Jangwani.

Simba ilipozuiwa usiku huohuo ikashusha msimamo wake kwamba haitacheza mechi hiyo ikidai ilinyimwa haki yake ya msingi ya kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi hiyo ikiwa kama timu mgeni kama ambavyo kanuni za ligi zinasema.

Wekundu hao walidai makomandoo wa Yanga na Meneja wa Uwanja wa Mkapa ndio waliosababisha kukosa kufanya mazoezi kwenye uwanja huo huku wenyeji wao wakisisitiza kwamba mchezo huo utachezwa kama ambavyo ulipangwa ingawa haukuchezwa. Yanga waliingiza timu uwanjani na wakapasha misuli kisha kurejea kwenye mabasi kurudi kambini.

CA 01

Baada ya uamuzi huo wa Simba, mapema asubuhi Machi 8, Bodi ya Ligi kupitia Mwenyekiti wake, Steven Mnguto ilisisitiza kwamba mchezo huo bado upo huku akiwataka mashabiki kwenda uwanjani akieleza kwamba Kamati ya Usimamizi wa Ligi itaketi siku hiyohiyo kutoa msimamo wa barua hiyo ya Simba.

Kikao hicho kilipoketi kamati hiyo ikashtua na kuja na uamuzi wa kuahirisha mchezo huo namba 184 ikisema inataka kufanyia kazi matukio ambayo yaliyojitokeza kwa kina, uamuzi ambao uliwakera wenyeji wa mchezo huo Yanga ambao bado ikapeleka timu yake uwanjani kisha ikafanya mazoezi licha ya mchezo huo kufutwa.

CA 03

Siku moja baadaye, Machi 9 Yanga ikatoa msimamo wake uliokuwa na maazimio matatu kufuatia kikao chao cha dharura cha Kamati ya Utendaji ikitaka kupewa ushindi kwenye mchezo huo ulioahirishwa, ikisema pia kwamba haitakubaliana na tarehe mpya ya mnchezo huo huku pia ikiitaka Bodi ya Ligi na TFF kuwawajibisha viongozi wanaosimamia Kamati ya Usimamizi wa Ligi na kuteua wengine kwa kile ilichodai kukosa weledi.

CA 05

leo mchana Yanga ikaweka wazi kwamba haikuridhishwa na majibu ya bodi ya ligi juu ya barua yao na kuamua rasmi kufungua kesi hiyo CAS.

Taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata zinasema kuwa kwenye barua hiyo Yanga kwa bodi imejibiwa kwamba maamuzi ya kamati hiyo yalikuwa halali na kwamba yalifikiwa kutokana na kuonekana viashiria vya ufunjifu wa amani huku ikisema mchezo huo utapangiwa tarehe mpya.

Mwanaspoti limejiridhisha jana kutokana kwa viongozi wa Yanga kwamba imeshafungua kesi hiyo CAS ikijibiwa kwamba kila kitu kimeshapokelewa nyaraka zao pamoja na malipo yao ambapo sasa watapangiwa tarehe ya kusikiliza shauri hilo.

Mwanaspoti liliwatafuta viongozi wa Yanga kuzungumzia hatua hiyo lakini waligoma kujiweka hadharani huku bosi mmoja wa juu akithibitisha kwa kusema kwamba:”Waulizeni bodi na TFF watajulishwa na CAS lakini sisi tumeshakwenda kutafuta haki yetu huko, tumechoshwa na kuburuzwa na kufedheheshwa kwa mambo ambayo yapo wazi yalihitaji usimamizi wa kanuni tu,”alisema bosi huyo wa juu ndani ya Yanga.

Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu wikiendi iliyopita aligusia taarifa hiyo ya Yanga; “Siyo CAS tu hata wakienda spidi.” wao hawana hofu.

“Kutamani ni sifa ya mwanadamu, anaweza kutamani kitu chochote. Hivyo, wacha waendelee kutamani. Sio CAS tu, hata wakienda Spidi.”

CA 02

Kufungua tu kesi CAS inahitajika uwe umeweka kiasi cha Dola 46,000 (Sh121 Milioni ) ambazo tajiri  wa Yanga alishazilipa.

Ingawa Yanga haitaki kulizungumzia hilo hadharani, lakini Mwanaspoti linafahamu jopo la wanasheria wao limeshajiandaa kwa shauri hilo.

Related Posts