Mjadala kuhusu Veta wamuibua Majaliwa, atoa maelekezo

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mjadala ulioibuka kuhusu ushauri alioutoa kwa wahitimu wa vyuo vikuu kwenda kupata ujuzi vyuo vya ufundi stadi (Veta) una tija.

Amesema mjadala huo una mambo mazuri ya kuishauri Serikali namna ya kuboresha mfumo wa ufundi stadi nchini, akiagiza watendaji kuchukua yaliyo mazuri yanayoshauriwa kupitia mjadala huo.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Machi 18, 2025, jijini Dar es Salaam, alipofungua maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishiwa kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta). Maadhimisho yatahitimishwa Machi 21.

“Tumieni fursa ya maadhimisho haya kuweka mwelekeo wa kitaifa, kutoa ushauri namna ya kuboresha mfumo wa ufundi stadi nchini. Mnaoendesha vyuo mna fursa ya kueleza changamoto na Veta yenyewe ina fursa ya kueleza changamoto na namna ya kuzitatua.

“Mjadala unaoendelea mtaani, Serikali ichukue yale yote bora yatakayoboresha mfumo wetu wa ufundi stadi. Mimi ninaufuatilia, hakika una tija kwa sababu kuna watu wanapinga na wengine wanashauri namna ya kwenda vizuri, kwa hiyo tutumie maadhimisho haya ambayo yamekuja wakati mzuri kukiwa na mjadala huu,” amesema.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Majaliwa akiwa ziarani wilayani Nzega mkoani Tabora, alizungumzia umuhimu wa Veta kwa wahitimu wa vyuo vikuu na kuibua mjadala mkubwa, uliojengwa kwenye dhana ya usomi na elimu ya Veta.

“Veta ile si tu kwa kijana wa darasa la saba, hata wewe uliyemaliza digrii, mtaalamu wa kompyuta, nenda kajifunze kushona nguo uwe fundi cherehani, nenda kajifunze ufundi umeme uwe fundi umeme,” alisema Majaliwa na kuongeza:

“Kwa hiyo, mwanafunzi wa chuo kikuu anaweza kwenda kusoma Veta kwa sababu pale anasomea ufundi na ndiyo malengo ya Serikali ya kutoa fursa ya watu kusomea ujuzi na ufundi, ili uwasaidie kujianzishia shughuli za kiufundi ambazo zitakuletea kipato na kuendesha maisha yako.”

Kauli hiyo, iliibua mjadala na wapo walioipokea kwa mtazamo hasi, kwamba Serikali inaishusha hadhi elimu ya chuo kikuu.

Hii ni kutokana na dhana potofu kwamba elimu ya ufundi stadi ni kwa waliokosa fursa ya kusoma elimu ya juu, mtazamo ambao wadau wa elimu wanasema unapaswa kubadilika.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, akizungumza katika maadhimisho ya Veta, amesema baada ya kumaliza elimu ya chuo kikuu alirudi Veta kupata ujuzi.

“Baada ya kumaliza shahada yangu ya ualimu nilikwenda Veta, kiu yangu ilikuwa kufahamu kushona viatu, wakati nasoma ilikuwa ni nadra kumuona mwanafunzi anavaa viatu na sasa natekeleza lengo langu la kushona viatu vya ngozi,” amesema.

Waziri Mkuu, Majaliwa, ameitaka Veta na taasisi nyingine zinazotoa mafunzo ya ufundi nchini kuhakikisha yanazingatia soko la ajira kwa kufanya tafiti kwa ushirikiano na Serikali, sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.

Ameitaka Veta kujiimarisha kuendana na mabadiliko ya teknolojia, akizisisiza taasisi zote za ufundi stadi kushirikiana na viwanda na waajiri ili kutoa wahitimu washindani kwenye soko la ajira.

“Niwahamasishe kampuni na taasisi binafsi kuendelea kutoa mafunzo na uzoefu wa kazi kwa wahitimu wetu, pia waruhusu wanafunzi wetu kuendelea kujitolea katika maeneo ya kazi, ikiwa ni mafunzo kwa vitendo ili kupata wafanyakazi walio bora,” amesema.

Majaliwa ameelekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuhakikisha vyuo 65 vya Veta vinavyojengwa nchini vinakamilika kwa wakati.

Ili kukuza ujuzi, Majaliwa ameitaka Veta kushirikiana na viwanda, waajiri, mashirika na taasisi za dini ili vijana wanaohitimu waendane na soko la ajira.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali inatoa ruzuku kwa vyuo vya Veta, mchango unaoonekana katika gharama za masomo.

Amesema kwa anayesoma Veta, ada yake ni Sh120,000 kwa mwanafunzi anayelala, kula na kusomwa chuoni, na kwa anayesoma na kurudi nyumbani ada ni Sh60,000.

Related Posts