RC awashukia wanaokwamisha usajili stakabadhi ghalani

Shinyanga. Wakati Serikali ya Mkoa wa Shinyanga ikiwaonya baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wanaokwamisha mfumo wa stakabadhi ghalani, wenyewe wamedai unachelewesha malipo na kuwakwamisha kiuchumi.

Sintofahamu hiyo imetokana na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ambaye amesema kutojisajili kwa baadhi ya wakulima kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani kunakwamisha juhudi za Serikali za kuwainua kiuchumi wakulima wadogo.

Macha ametoa kauli hiyo leo Machi 18, 2025 katika kikao na wakulima na wafanyabiashara wa mazao ya dengu, choroko na mchanganyiko kilichofanyika katika ofisi ya mkuu wa mkoa iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Macha amesema baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wamekuwa wakikwamisha kwa makusudi usajili kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani, kitendo kinachokwamisha juhudi za Serikali za kuwakwamua kiuchumi wakulima wadogo.

 “Baadhi yenu elimu tuliotoa imezaa matunda, lakini kuna wengine wana uelewa kuhusiana na huu mfumo wa stakabadhi ghalani, lakini ni makusudi tu hawataki kujisajili ili kuisumbua Serikali, hatua kali zitachukuliwa watakapobainika,” amesema Macha.

Amesema wakulima wengi wanaotumia mfumo huo wamefanikiwa kupata bei nzuri kwa mazao yao na kuwa na uhakika wa malipo, lakini bado kuna changamoto kutokana na baadhi ya wakulima kutokujisajili.

Moja ya ghala lilipo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Picha na Hellen Mdinda.

Macha amesema wakulima hao wanasababisha  kikwazo kwa Serikali katika juhudi zake za kuboresha hali ya maisha ya wakulima wadogo, kwa kuwa wanakosa fursa za kupata mikopo, uhifadhi bora wa mazao, na njia bora za kuuza.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima akiwamo Shija Lameck wamesema  kutumia mfumo huo ni kama kuwadidimiza wakulima kiuchumi, kwa sababu itabidi asubiri siku ya mnada ndio alipwe fedha yake, wakati nje ya mfumo angeuza na kulipwa moja kwa moja na kuondoka.

“Tukitumia mfumo huu inatulazimu tusubiri hadi siku ya mnada ndio tulipwe pesa zetu ni bora tuuze kama tulivyozoea kwa sababu mtaji wetu ni mdogo na kuna matumizi pia hatuwezi kusubiri mnada” amesema Lameck.

Mkulima mwingine wa zao la dengu, Alfred Joakim amesema kuwa kutumia mfumo huu ni ngumu kwa sababu mnada wenyewe unafanyika mara moja kwa wiki, inakuwa ngumu katika biashara kusubiri wiki hadi wiki.

“Bora tuachane na mfumo kwa sababu ni ngumu kufanya biashara ya mara moja kwa wiki wakati mitaji yetu inabidi iwe kwenye mzunguko kila siku ili kuzalisha zaidi, kutokana na hivyo bora tuendelee na biashara kama siku zote,” amesema Joakim.

Mkulima mwingine wa mazao mchanganyiko, Omari Juma ameshauri kuwa wakulima wenye uelewa wawe chachu ya kuwavuta wengine kujisajili waweze kunufaika kupitia mfumo huu.

“Kwa sisi tuliojisajili na kuona faida ya huu mfumo wa stakabadhi ghalani tuwe chachu kuwavuta wakulima wenzetu ambao bado hawajajisajili ili na wao wanufaike” amesema Juma.

Mfanyabiashara kutoka Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni mnufaika na mmiliki wa ghala, Hassan Mboje ameeleza faida ya kutumia mfumo huu ikiwa ni pamoja na kuongeza pato litakaloweza kumuinua mkulima mdogomdogo,

“Kupitia mfumo huu mkulima hatouza mazao yake kwa bei ya hasara mfano zao la dengu kwa mkulima mwenye uelewa na huu mfumo anauza kwa mnunuzi kilo moja Sh1,200 na mnunuzi anauza Sh1,300, lakini kwa mkulima asiyeelewa anauza kwa bei ya hasara hadi Sh600 kwa kilo moja na mnunuzi anauza Sh1,300 ambapo atanufaika mara mbili huku mkulima akinyonywa” amesema Mboje.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani, Asangye Bangu amesema kuwa kabla ya kuweka mazao kwa ajili ya mnada huwa yanasafishwa kutenganisha uchafu ili kupata uzito sahihi.

“Kabla ya kupaki mazao kwa ajili ya mnada huwa tunasafisha kwa kuchekecha kwenye chekecheo kubwa ili kuyatenganisha na mchanga hii inasaidia kupata uzito sahihi,” amesema Bangu.

Related Posts