Dar es Salaam. Kesi ya jinai inayowakabili meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai na mwanaharakati Godlisten Malisa, imekwama kusikilizwa kutokana na upande wa mashitaka kukosa shahidi mbadala baada ya aliyekuwa ameandaliwa kushindwa kupanda kizimbani akidaiwa kuugua ghafla.
Katika kesi hiyo, Boni Yai, mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kutoa taarifa za uongo mitandaoni.
Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao yao ya kijamii ya X na Instagram, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.
Katika taarifa hizo wanadaiwa kulihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia akiwemo mkazi wa Dar es Salaam, Robert Mushi, maarufu Babu G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Omari Msemo.
Kesi hiyo ya jinai inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilitarajiwa kuendelea kusikilizwa leo, Machi 18, 2025.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imeshindwa kuendelea na usikilizwaji baada ya shahidi wa tatu wa upande wa mashitaka aliyekuwa ameandaliwa licha ya kufika mahakamani hapo, lakini ameshindwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi kwa kile kilichodaiwa kuugua ghafla muda mfupi kabla ya kesi kuanza.
Kesi hiyo ilipoitwa, mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Cuthbert Mbilingi ameieleza Mahakama kesi hiyo ilikuwa imepangwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na walikuwa na shahidi mmoja.
“Lakini shahidi tuliyemtarajia alifika mahakamani lakini akapata dharura kwani amejisikia vibaya kiafya. Hivyo tunaomba tupangiwe tarehe nyingine ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hili,” amesema Wakili Mbilingi.
Hoja hiyo ya kuahirisha shauri hilo, imepingwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala kuwa haina msingi na anaiomba Mahakama iikatae.
Wakili Kibatala amesema kesi hiyo inachukuliwa kama ni moja ya mashauri ya muda mrefu na ilipangwa kwa siku mbili mfululizo, yaani jana Jumatatu Machi 17 na leo 18, 2025.
Amesema jana walikuwepo na mawakili wa Serikali na kesi ikapangwa kwamba itaendelea leo saa 5:00 na walitarajia kuwa upande wa mashitaka walete shahidi zaidi ya mmoja.
Kuhusu hoja ya kuahirisha kwa sababu ya dharura ya shahidi, Wakili Kibatala amesema ingawa hilo ni suala binafsi lakini walitarajia upande wa mashitaka ufafanue zaidi.
“Tulitarajia waende mbali zaidi, kwamba labda kaumwa ghafla, kafiwa ghafla, au kaunguliwa na nyumba ghafla au kagoma kutoa ushahidi ghafla,” amesema Wakili Kibatala na kuhitimisha:
“Kwa hiyo tunapinga kuahirisha kesi hii kwa leo, wenzetu wapewe muda watafute shahidi ili tuendelee.”
Hata hivyo, Wakili Mbilingi, akijibu hoja za Wakili Kibatala amesema aliweka wazi tangu mwanzo kuwa shahidi alijisikia vibaya kiafya.
Wakili Mbilingi amesema katika mwenendo wa kesi hiyo na hata siku kabla ya jana wakati mwingine washtakiwa walikuwa hawafiki mahakamani na walikuwa wanatoa sababu na wao, licha ya kuwa mashahidi walikuwa wanatoka mbali huku wakilipwa lakini walikuwa wanaahirisha kesi.
Hivyo amehoji itashindikanaje leo kuahirisha na kupangiwa tarehe nyingine?
“Kwa hiyo tunasisitiza tupangiwa tarehe nyingine,” amesema Wakili Mbilingi na kuongeza:
“Shahidi wetu wa pili ni askari alipata msiba tangu jana kwa hiyo amekwenda kwenye msiba. Huyo shahidi mwingine hatuwezi kumtafuta na kumuandaa sasa hivi. Kwa hiyo tunasisitiza tupangiwe tarehe nyingine ili tuweze kuendelea na shauri.”
Hakimu Swallo baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema ni kweli shauri hilo limeshakuwa la muda mrefu na Mahakama ilitoa maelekezo kuandaa mashahidi ili kuhakikisha linamalizika haraka.
“Kutokana na maelezo kuwa shahidi wao (upande wa mashitaka) ana dharura, kwa masilahi ya haki nitatoa ahirisho la mwisho na wakati ujao upande wa mashitaka waandae mashahidi zaidi ya mmoja,” amesema Hakimu Swallo.
Hivyo Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 3, 2025 kesi hiyo itakapoendelea kusikilizwa kuanzia shahidi wa tatu wa upande wa mashitaka.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Mei 6, 2024 na kusomewa jumla ya mashitaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake huku Malisa akikabiliwa na shitaka moja, ambalo ni taarifa wanazodaiwa kuzichapisha mitandaoni kwa tarehe tofautitofauti.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 jijini Dar es Salaam.