Rungwe. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amemtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kufanya mazungumzo na kampuni ya Mohammed Enterprises ili irejeshe mashamba ya chai ya Rungwe kwa wananchi kama imeshindwa kuyaendeleza.
Msingi wa kuzungumza hivyo ni baada ya wananchi wa Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, kumweleza kiongozi huyo kuwa ni muda mrefu tangu kampuni hiyo ilipochukua eneo hilo kutoka kata tano kwa ajili ya kuzalisha zao la chai, lakini ameyatelekeza, hakuna shughuli inayofanyika.
Wakiwasilisha kero hiyo, wananchi hao wamedai kinachowaumiza zaidi ni kwamba katika eneo hilo kuna nguvu kazi kubwa, lakini inashindwa kufanya shughuli za kilimo kwa kukosa ardhi.
Akizungumza na wananchi hao leo, Jumanne, Machi 18, 2025, Wasira amewaahidi kuwa anakwenda kuzungumza na Waziri Bashe, kushughulikia tatizo hilo. Amesema kuwa mwekezaji akishindwa kuendeleza ardhi, Rais ana uwezo wa kuitwaa.
“Namuagiza Waziri wa Kilimo achukue hatua ya kumaliza jambo hilo haraka, ili ardhi iweze kutumika. Kwanza, katika mazingira ya huku Rungwe, ardhi ni ndogo, inakuwaje wewe una eneo kubwa halafu hulitumii? Hiyo ni dhambi. Nitazungumza naye leo hii ashughulikie suala hili.
“Tulikupatia mashamba ulime zao la chai. Ukiacha kufanya hilo, unavunja mkataba. Hakuna mtu anayeruhusiwa kumiliki ardhi na kuiacha bila kuitumia, halafu aseme ana haki miliki na ardhi ile,” amesema.
Wasira amesema ndiyo maana baada ya kupata uhuru walikataa sheria za wakoloni (Free Hold) kwa sababu ilikuwa inampa mtu haki ya kumiliki ardhi milele hata kama haitumii kufanya shughuli yoyote.
“Baada ya kuikataa sheria hiyo ya kikoloni, tulianzisha ya kwetu ambayo kama unachukua ardhi, lazima ufanye kile ulichoahidi kufanya. Sasa kuna Mohammed Enterprises, tangu muda mrefu mashamba yamekuwa pori. Tunataka kuiambia Serikali kupitia Waziri wa Kilimo kuwa kama mwekezaji huyo ameshindwa kufanya kazi na ardhi haizalishi, basi airudishe,” amesema.
Wasira amesema ni lazima Serikali ijue cha kufanya kwa sababu sheria ya kumiliki ardhi inasema lazima izalishe. Kama inakuwa tofauti na hilo, tafsiri yake ni kudumaza uchumi wa zao husika.
“Hatuna mgogoro naye, lakini shida yetu ni utekelezaji wake. Ardhi ile ameitelekeza na tuna shida naye katika kuitelekeza sheria ya ardhi aliyokodishwa. Ifahamike ardhi ni mali ya Watanzania wote, na Rais amepewa mamlaka ya kuisimamia kwa niaba ya wananchi,” amesema Wasira.
Awali, mkazi wa Ngendera, Athony Kagura, amesema eneo hilo lilichukuliwa tangu mwaka 1974, lakini limetelekezwa na limekuwa sehemu ya kuishi wanyama wakali kama chatu na wengine ambao ni hatari zaidi.
“Kiongozi unapita njia unaenda Kyela, utaona mashamba makubwa yametelekezwa. Idadi ya watu inaongezeka, na vijana hawana sehemu ya kufanya kazi wala kuishi. Mashamba yarejeshwe watu wafanyie kazi. Ilivyo sasa, hayana tija,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Richard Kasesela, amesema ni mzaliwa wa eneo hilo na anajua wananchi wake wanakabiliwa na tatizo la uchumi.
“Eneo hilo lina vijana wengi wa kufanya kazi ya kilimo ili kuzalisha mazao mbalimbali, ikiwemo parachichi na chai. Ni lazima Serikali iangalie namna ya kuwainua ili wafanye kazi ya kuliingizia Taifa kipato,” amesema Kasesela.