Mambo matano yatakayomuinua mwanamke kiuchumi

Dar es Salaam. Hali ya kiuchumi ya mwanamke inategemea mambo mengi, lakini baadhi ya vipengele muhimu vinavyochangia mafanikio ni elimu, nidhamu, kujituma, kujiamini na uwepo wa rasilimali.

Haya yamejidhihirisha kama silaha muhimu zinazoweza kumuinua mwanamke kiuchumi na kumwezesha kushiriki kikamilifu katika jamii.

Kauli hiyo imeelezwa leo Machi 18, 2024 jijini Dar es Salaam na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika mkutano ulioandaliwa na Studiored Communications, kujadili fursa na changamoto zinazomkabili mwanamke haswa katika upande wa uchumi.

Balozi Mulamula amesema elimu ni muhimu katika kumfanya mwanamke kutumia vyema fursa na rasilimali anazozipata kujiimarisha kiuchumi.

“Ili kudumu katika nguvu ya kiuchumi elimu ni muhimu hata ya msingi au ya ujuzi fulani itakusaidia kupiga hatua zaidi,” amesema.

Balozi Mulamula amesema si vibaya kwa mwanamke kupata elimu juu ya masuala mbalimbali ambayo yatamsaidia kuongeza maarifa katika kile anachokifanya

Pia, amegusia suala la uwepo wa rasilimali ikiwemo fedha, akieleza kuwaunganisha wanawake na rasilimali za kifedha ni muhimu kunaweza kuwasaidia kukidhi mahitaji yao ya msingi na kuanzisha au kukuza biashara.

“Kama hauna fedha au rasilimali muhimu mwanamke atainukaje? ni ngumu kuinuka,” amesema.

Balozi Mulamula amehimiza wanawake kujitokeza kwa wingi ili kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwezesha kufikiwa kwa usawa wa kijinsia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Studiored  Communications, Doris Rebangira amesema kuwa hayo yote hayawezi kufanikiwa kama mwanamke hatajituma na kuwa na nidhamu katika kile anachokifanya.

Rebangira amesema ili mtu aweze kufanikiwa katika jambo analofanya ni muhimu kuweka nidhamu na jitihada.

“Hakuna mafanikio yanayokuja ndani ya usiku mmoja, inahitaji kuwa mvumilivu, kutokata tamaa, kuweka malengo na jitihada kwa kile unachokifanya,” amesema.

Amesema kuwa suala la kumuwezesha mwanamke kiuchumi linaanzia katika ngazi ya familia katika malezi.

“Ni vyema jamii ikaachana na zile dhana potofu kuwa mwanamke hawezi, mambo yamebadilika,” amesema.

Kwa upande wake, Asia Kiwori ambaye ni mmoja wa washiriki wa kongamano hilo amewasihi wanawake kuacha kubweteka wanapoingia kwenye ndoa, wafanye kazi ili kujiimarisha kiuchumi na kuongeza pato la familia.

“Baadhi ya wanawake wakiolewa ndio wanaona wamemaliza, kila kitu atafanya mwanaume nyakati zimebadilika, umewahi kuwaza akiugua au kufariki utaishije wewe na watoto wako,” amehoji.

Related Posts