Kahama. Idadi ya watoto wanaozaliwa katika Hospitali ya manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kwa siku ni 20 hadi 25, kwa mwezi ni watoto 675, jambo ambalo limetajwa kusababisha msongamano mkubwa kwenye wodi ya mama na mtoto hospitalini hapo.
Kutokana na hali hiyo akina mama wanaojifungua watoto njiti kwenye hospitali hiyo wanakosa sehemu yenye stara kwa ajili ya kangaroo, huku wakati mwingine wakilazimika kuhamishwa kutoka jengo moja hadi jingine kwa machela wakiwa na maumivu makali ya uzazi.
Ili kukabiliana na adha hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama kupitia mapato ya ndani, imeanzisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto, lenye thamani ya zaidi ya Sh6.7 bilioni, litakalokuwa na uwezo wa kubeba vitanda 148.
Jengo hilo la ghorofa, ni maalumu kwa ajili ya mama na mtoto, litakuwa na sehemu ya kuhifadhi watoto njiti na sehemu ya kufanyia kangaroo kwa watoto hao.
Eneo lingine ni sehemu ya akina mama kupumzikia wakisubiri kujifungua (mama ngojea), sehemu ya kujifungulia, sehemu ya kupumzika baada ya kujifungua wakisubiri kuruhusiwa pamoja na eneo la upasuaji.
Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga, Salome Makamba, akizungumza leo Machi 18, 2025 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tamisemi ilipotembelea na kukagua jengo hilo, amesema ujenzi wa jengo hilo ni mkombozi kwa akina mama wanaojifungua hospitalini hapo.

Meneja wa mradi wa Manispaa ya Kahama Mashala Mboje amesema, akiielezea kamati ya kudumu ya Bunge ya Tamisemi kuhusu ramani ya jengo la mama na mtoto manispaa ya Kahama litakalokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya 100 kwa siku, linalojengwa kwa gharama ya Sh6.7 Bilioni fedha za mapato ya ndani. Picha na Amina Mbwambo
Amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kutimiza azma ya Serikali ya kuweka mazingira bora na yenye staha kwa ajili ya mama na mtoto.
“Leo ninaonyesha furaha kubwa kwa niaba ya wanawake wenzangu wengi, tuliopata bahati ya kujifungulia kwenye hospitali hii ya manispaa ya Kahama, na mimi ni mmoja wao, na likikamilika hili jengo tutaweza kujifungua kwenye mazingira yenye staha, ya kutustiri sisi wanawake na uanauke wetu,” amesema Makamba.
Mbunge wa jimbo la Kahama mjini Jumanne Kishimba amesema idadi hiyo ni ile ya wanawake wanaofika hospitali, lakini jamii ya Kisukuma bado wapo wanaojifungulia nyumbani na baadaye kufikishwa hospitali, hivyo idadi ya wanaozaliwa kwa mwezi ni takriban watoto 1,000.
Amesema kutokana na jiografia ya manispaa hiyo kuzungukwa na migodi midogo, idadi ya watu inaongezeka kila siku kutokana na wahamiaji kuwa wengi, hivyo ameiomba Serikali kuongeza bajeti kwa hospitali hiyo.
Naibu Waziri ofisi ya Rais Tamisemi, Zainab Katimba amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali imewekeza kiasi cha Sh1.29 trilioni kwenye sekta ya afya, na sasa itaongeza nguvu kwenye jengo la mama na mtoto Kahama ili likamilike haraka na kuwahudumia wananchi.
“Halmashauri wana wajibu wa kuanza ujenzi wa miradi hii mbalimbali ya maendeleo, lakini sisi kama Serikali kuu tunakuja kuongeza nguvu ili kuhakikisha jengo hili linakamilika,” amesema Katimba.
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Meneja wa mradi wa Manispaa ya Kahama, Mashala Mboje amesema, ujenzi wake ulianza Julai 15, 2022 na unatarajia kukamilika Julai mwaka huu, na linajengwa na mkandarasi Suma JKT ya Geita kwa gharama ya Sh6.79 bilioni fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.
Kwa upande wake kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kahama, Dk Baraka Msumi amesema kukamilika kwa jengo hilo ni mkombozi kwenye huduma za mama na mtoto hospitalini hapo, kwani litaondoa msongamano mkubwa uliopo sasa.