Mwanza. Watu wenye ulemavu wamelalamikia ukiukwaji wa Sheria ya Ajira inayoelekeza kampuni na mashirika kuajiri angalau wafanyakazi watatu wenye ulemavu kati ya 20 kuwa haizingatiwi.
Pia, wamelalamikia ushirikishwaji mdogo kwenye fursa za kimaendeleo zinazotolewa na Serikali na wadau wa maaendeleo pamoja kukithiri kwa baadhi ya vitendo vya ubaguzi.
Wakizungumza leo Jumamosi Mei 18, 2024 kwenye Kongamano la Uchumi kwa Watu Wenye Ulemavu lililoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata) Wilaya ya Nyamagana wameiomba Serikali kuunda chombo maalumu kitakachokuwa kinasimamia sheria hiyo ya ajira.
“Kwenye ajira kuna sheria inayozitaka kampuni ya binafsi na Serikali zinapokuwa zinatoa ajira kati ya wafanyakazi 20 watatu lazima wawe walemavu japo kuwa hili kwa walemavu bado haijafahamika sana lakini imekuwa changamoto kubwa kwa sababu sheria hiyo haifuatwi,” amesema Jane Maila Mwenyekiti Idara ya Wanawake na Watoto Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata).
“Kwa upande wa serikalini vijana wengi walemavu wamesoma na kumaliza shahada zao lakini bado hawajapata fursa,” amesema Maila.
Mwanachama wa Chawata, Nyamulanga Lwakatale amewataja waajiri kuwa sababu ya kutofuata sheria hiyo huku akidai kuwa hata wachache wanaopata ajira hukumbana na mazingira magumu ya kazi hivyo kuiomba Serikali kuliangalia hilo.
“Serikali inajitahidi sana kwenye suala la ajira ila shida ipo huku chini kwenye utekelezaji, sheria inasema vizuri lakini waajiri hawafuati kabisa na hata mlemavu anaweza kuajiriwa, lakini unakutana mazingira magumu ya kazi,” amesema Lwakatale.
“Naishauri kiundwe chombo huru kitakachokuwa kinazunguka kwenye mashirika na taasisi zote ambazo hazifuati sheria ya ajira ya kuajiri angalau watatu kati ya wafanyakazi 20 na chombo hicho kiundwe na wanasheria, viongozi kutoka serikalini pamoja na walemavu,” amesema Lwakatale.
Mwenyekiti Shivyawata Wilaya ya Nyamagana, Hamza Nyamakula amesema mbali na Serikali kujitahidi kuboresha miundombinu mbalimbali nchini bado suala la upatikanaji wa ajira umekuwa mgumu kwa kundi hilo kutokana na mitazamo hasi kuhusiana na wao.
“Upatikanaji wa ajira nchini umekuwa mgumu sana hii ni kutokana na mitazamo hasi ambayo imejengeka vichwani kwa watu au waajiri tunaomba sana wawe na mitazamo chanya kuhusu kundi hili kwa kuwa wao wana uwezo wa kufanya kazi kama wengine lakini pia wajue na wao wana maarifa kama wao,” amesema Nyamakula.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (Tas), Alfred Kapole amesema ili kuondokana na changamoto ukosefu wa kipato na utegemezi kwa watu wenye ulemavu, Serikali iongeze fungu la asilimia 10 la mikopo inayotolewa katika halmashauri kwa kuwa haitoshi.
“Zile asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu kutoka kwenye asilimia 10 ambayo imegawanya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu iongezwe kwa sababu kuna baadhi waliopata wamefanya maendeleo makubwa sana, kwa hiyo na wengine wakipata itasaidia kuwainua kiuchumi na kuachana na tabia ya kuomba omba,” amesema Kapole
Akijibu changamoto hizo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Godfrey Chambo amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kufanya mapitio na kuboresha Sera ya Taifa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 ili iendane na mazingira ya sasa.
“Tunafahamu sera inatoa wigo mpana kwa masuala mbalimbali na wadau ili waweze kushiriki afua mbalimbali za utatuzi wa changamoto za watu wenye ulemavu, kwa hiyo kwa sasa tumefanya tathmini ya sera hiyo katika maeneo mbalimbali,” amesema Chambo.
Mkuu wa Wilaya Ilemela, Hassan Masala ametoa wito kwa watu wenye ulemavu kuzingatia taratibu na maagizo yanayotolewa katika uombaji wa ajira zinapokuwa zinatangazwa.
“Serikali imeweka msisitizo kwa mwombaji aweze kujieleza ulemavu alionao ili aweze kurahisisha uchambuzi wa maombi hayo lakini suala hili limekuwa ni changamoto, hivyo kusababisha baadhi ya waombaji kukosa nafasi hizo,” amesema Masala.