Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo, Jumanne Machi 18,2025 kimetoa siri kuhusiana na mkutano wao na msajli wa vyama vya siasanchini.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kimemueleza Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusiana na msimamo wao wa ‘No Reform, No Election’ unaolenga kushinikiza mageuzi makubwa ya mifumo ya uchaguzi nchini.
Mnyika amesema katika mazungumzo yao na msaliji wa vyama vya siasa Jaji, Mutungi , wamemueleza kwamba endapo mageuzi hayo hayatafanyika basi chama hicho kimejipanga kuzuia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari nje ya viunga vya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa muda mfupi baada ya kutoka kwenye ofisi hizo, Mnyika amesema viongozi wa chama hicho wamelazimika kufika kwenye ofisi hizo kufuatia wito walioupokea hivi karibuni ambao pamoja na mambo mengine uliwataka kufika hapo ili kueleza wanamaanisha nini wanaposema ‘No Reform, No Election’
Kupitia kikao hicho kilichochukua zaidi ya saa nne, Mnyika amesema viongozi wa chama hicho wameieleza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa kauli hiyo hawajaitoa kwa bahati mbaya kwani kwa muda mrefu nchini kumeshuhudiwa chaguzi ambazo zisizokuwa huru na haki zisizoheshimu maoni ya wananchi wanayotoa kupitia masanduku ya kura, na kwamba mara zote imeelezwa na wadau mbalimbali kuwa suluhisho ni kufanyika kwa mageuzi ya mifumo ya uchaguzi ikiwemo kupatikana na Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi, jambo ambalo linaonekana kupigwa chenga na watawala.
“Sisi tunaamini baada ya kutuita na sisi kuitikia wito wao, sasa wanapaswa kuyachukulia kwa uzito tuliyowaeleza ili na wao (Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa) wawe na mchango kama wadau wengine tuliokutananao, mchango wa kuwezesha kufanyika kwa mageuzi na mabadiliko kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025, bila mabadiliko hakuna uchaguzi No Reform, No Election,” amesema Mnyika.
Hata hivyo, Mnyika amesema taasisi hizo mbili Chadema na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa baada ya kikao hicho wanatarajia kukutana tena hivi karibuni kwa muendelezo wa mazungumzo hayo.
Stori na Elvan Stambuli, GPL